Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 27, 2024 Local time: 02:38

Miguna asema alidungwa sindano na kupoteza fahamu


Wakili mzaliwa wa Kenya, Miguna Miguna, akiwa katika hospitali moja mjini Dubai.
Wakili mzaliwa wa Kenya, Miguna Miguna, akiwa katika hospitali moja mjini Dubai.

Mahakama ya juu nchini Kenya, Alhamisi iliwatoza faini ya shilingi 200,000 kila mmoja, maafisa watatu waandamizi wa serikali, kwa kukiuka maagizo ya mahakama kuhusu sakata ya wakili na mwanaharakati aliyeondolewa nchini humo, Miguna Miguna.

Siku ya Jumatano, mahakama hiyo iliwapata na hatia ya kukiuka maagizo ya mahakama waziri wa usalama wa ndani, Fred Matiang'i, inspekta mkuu wa polisi, Joseph Boinett na mkurugenzi wa idara ya uhamiaji, Gordon Kihalangwa, kati ya wengine.

Hayo yalijiri huku Miguna, kupitia ujumbe kwa vyombo vya habari kutoka mjini Dubai, akisema kwamba alidungwa sindano kwenye mikono na miguu akiwa kwenye uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta na baadaye akapoteza fahamu kabla ya kuwekwa kwenye ndege na kupelekwa mjini Dubai kinyume na matakwa yake.

Wakili huyo alisema alikataa kwendelea na safari hadi London kwa sababu alikuwa mgonjwa. Mwanaharakati huyo aliyezua utata alituma picha zilizomuonyesha akiwa kwenye hospitali moja mjini Dubai.

"Nimefanyiwa vipimo na kuonyesha kwamba nilidungwa kwa dawa iliyonifanya nipoteze fahamu kabla hawajaniweka kwa ndege kwa lazima," alisema Miguna.

"Ndege ilipotua saa kumi na moja na dakika ishirini na tano asubuhi, niliamka na nikamuuliza mtua aliyekuwa kando yangu na aliyekaa kama afisa wa Flying Squad tulikuwa wapi...akaniambia tuko Dubai," alisimulia Miguna na kuongeza kwamba alikataa kuondoka kwenye eneo la usafiri wa kimataifa hadi apelekwe hospitali, na baadaye arudishwe nchini Kenya.

Wakati huo huo, tume ya kutetea haki za binadamu ya Kenya, KNHRC, Alhamisi iliishutumu hatua ya serikali ya nchi hiyo ya kumpeleka nje ya nchi kwa mara nyingine tena wakili huyo.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, tume hiyo aidha ilisema ni ukiukaji wa hali ya juu wa haki za binadamu, kwa serikali ya Kenya, kupuuza maagizo kadhaa ya mahakama ya juu, kuhusiana na sakata hiyo ya Miguna Miguna.

Mapema Alhamisi, kwa mara nyingine tena serikali ya kenya ilikaidi amri ya mahakama kuu iliyoitaka kumuachilia wakili huyo.

Miguna alikuwa amezuiliwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kwa zaidi ya saa 36.

Wakili huyo alithibitisha, kupitia taarifa kutoka Dubai, kwamba aliingizwa kwenye ndege ya shirika la ndege la Emirates iliyokuwa inaelekea Dubai, kinyume na matakwa yake.

Alisema kuwa sindano aliyodungwa ilimfanya kupoteza fahamu hadi alipowasili mjini Dubai na kuongeza kwamba wakatii wa kuandika taarifa hiyo, alikuwa na maumivu makali.

Alieleza kwamba hangekubali kuondoka Dubai iwapo ndege ambayo angeabiri haingekuwa inaelekea Nairobi.

Baadaye Miguna alituma picha zilizomuonyesha akiwa katika hospitali moja mjini humo.

Miguna alizuiliwa JKIA baada ya kuwasili kutoka Canada ambapo awali alirejeshwa huko kwa madai kuwa alikuwa ameukana uraia wa kenya.

Maafisa waandamizi wa serikali ya Kenya walitakiwa kufika mbele ya jaji hivi leo kueleza ni kwa nini walikiuka maagizo kumhusu wakili huyo.

Serikali imeshikilia kwamba Miguna si raia wa Kenya na ni lazima aombe viza ya kuingia nchini au aombe uraia wa nchi hiyo.

XS
SM
MD
LG