Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 16:46

Wafanyabiashara Kariakoo wataka Rais Samia akutane nao kutatua kero ya rushwa na mrundikano wa kodi


Wafanyabiashara wa Kariakoo wakiwa wanamsubiria Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amosi Makala.
Wafanyabiashara wa Kariakoo wakiwa wanamsubiria Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amosi Makala.

Mrundikano wa kodi zinazotozwa na mamlaka ya mapato Tanzania, TRA, dhidi ya wafanyabiashara pamoja na rushwa zimeelezwa kuwa ni miongoni mwa sababu zilizowafanya wafanyabiashara wa kariakoo kufanya mgomo kuanzia leo Jumatatu.

Wafanyabiashara hao wanasema wataendelea na mgomo mpaka pale watakapo kutana na Rais wa nchi huku wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wakiutazama mgomo huo endapo hauto malizika utasababisha athari kubwa ya kiuchumi.

Zimetumika dakika thelathini za kutatua mgomo wa wafanyabiashara wa Kariakoo dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amosi Makala, utatuzi ambao haukuleta matunda baada ya wafanyabiashara hao kubaki na msimamo wao wakutofungua maduka mpaka pale watakapo wezeshwa kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan.

Huku sababu ya mgomo huo ikitajwa ni ongezeko la kodi uwepo wa rushwa kwa baadhi ya viongozi wa mamlaka ya mapato Tanzania, TRA, pamoja na uanzishwaji wa kodi ya ghala imekuwa ni vikwazo vinavyo endelea kuwaadhibu wafanyabiashara hao ambao wamekata tamaa na kauli za viongozi kwa kuwa wamesha zungumza nao mara nyingi bila ya mafanikio yoyote.

Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo wamebeba mabango kueleza masikitiko yao juu ya madai ya kuwepo mrundikano wa kodi na rushwa.
Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo wamebeba mabango kueleza masikitiko yao juu ya madai ya kuwepo mrundikano wa kodi na rushwa.

Orokio Ombeni Katibu Mkuu wa wafanyabiashara katika Soko la Kariakoo amesema watafunga biashara zao mpaka pale watakapo onana na Rais Samia kwa kuwa Mkuu wa Mkoa hana mamlaka yeyote kwa kamishna wa kodi za ndani kuweza kumaliza tatizo lao.

Ombeni anaeleza: " Sisi tunafunga maduka labda Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania hana taarifa kwa hichi kinacho fanyika Kariakoo huu ujumbe umfikie Rais aweze kuelewa nini tatizo la wafanyabiashara kwahiyo inamaana unavyo zungumza na mkuu wa mkoa,mkuu wa mkoa kazi yake anapooza si kwamba anaweza akatatua kero za wafanyabiashara."

Ama wafanyabiashara hao kwa kauli moja mara baada ya Mkuu wa Mkoa kuondoka katika soko hilo walikubaliana kwa pamoja kufunga maduka yao kwa muda usio julikana licha ya Mkuu wa Mkoa kuwataka wafungue kwakuwa changamoto zao wameanza kuzifanyia kazi na kuwaahidi siku ya Alhamisi viongozi wa wafanyabiashara watakutana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Mkoani Dodoma katika mazungumzo yatakayo leta muafaka.

John Mbula miongoni mwa wafanyabiashara amesema biashara wanazofanya hazilingani na kodi wanazotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA, mamlaka hiyo imekuwa ni kero kwao huku wakiendelea kupokea rushwa pale mizigo yao wanapo ikamata kwa lengo la kunusuru biashara zao.

Mbula anasema: "Kero kubwa tunayoipata Kariakoo ni kodi za hawa TRA hatujui wanatumwa na nani atukuja hapa kumsikiliza mkuu wa mkoa wala waziri wa fedha tunaimani wanashirikiana na hawa TRA ili kutukandamiza sisi hapa ninapo ongea juzi nimekamatiwa mzigo wa mteja wangu nimetoa laki nane sijui kama ni kodi kwasababu TRA anavyo mkamata mteja wangu kinacho toka kwake ni namba na karatasi ya malipo."

Hata hivyo Joshua Lukonge mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akizungumza na VOA amesema suala la soko la Kariakoo limekuwa la muda mrefu hivyo pande zote mbili zinapaswa kukaa na kutatua changamoto zinazo jitokeza na kuweka nia ya dhati itakayoweza kulimaliza tatizo hilo linaloelekea kuathiri nchi kwa kiasi kikubwa.

Lukonge anasema: "Kwa hiyo hawa watu wawili ukiangalia wanahoja za msingi huyu anasema mfumo ni mgumu kwa hiyo sisi tunataka kupunguza mapato kuvuja, hawa wanasema hapana hakuna sababu yoyote ile hiyo mnatuonea mnataka mtulipishe kodi kwenye maduka mnataka mtulipishe kodi kwenye stoo serikali ikae chini na wafanyabiashara watatue wanao athirika ni wengi wengi mno."

Wakati mgomo huo ukiwa upo kwenye siku yake ya kwanza hii leo wajasiriamali katika soko hilo wameitaka serikali kutafuta ufumbuzi kwakuwa wao ndio watakao athirika kwa kiasi kikubwa kwani wamekuwa wakiyategemea maduka hayo katika kujipatia riziki.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Dar es Salaam, Tanzania.

XS
SM
MD
LG