Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 09:45

Wakulima waitaka serikali kuhakikisha bajeti ya 2023/24 inalenga mahitaji yao


Vijana wakiwa katika ufunguzi wa mashamba makubwa ya pamoja (Block Farms) Chinangali, Dodoma. Picha kwa hisani ya Ikulu, Dar es Salaam.
Vijana wakiwa katika ufunguzi wa mashamba makubwa ya pamoja (Block Farms) Chinangali, Dodoma. Picha kwa hisani ya Ikulu, Dar es Salaam.

Wakulima wameitaka serikali kuhakikisha bajeti itakayo pitishwa 2023/24 kulenga zaidi wakulima wadogo wadogo ambao wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali maeneo ya vijijini na kushindwa kufikiwa na wataalamu wa kilimo.

Hali hii imepelekea uzalishaji mdogo wa mazao kwa kukosa misaada ya kitaalamu huku wasomi wakionyesha kuridhishwa na makadirio ya bajeti hiyo.

Takwimu zinaonyesha asilimia 65.6 ambayo ni zaidi ya Watanzania milioni 40 maisha yao ya kila siku yanategemea kilimo huku kilimo kikionyesha kukua kwa asilimia 3.9 mwaka 2021 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.9 mwaka 2020 hata hivyo licha ya kuonekana kwa ukuaji wa kilimo bado wakulima wengi wameendelea kukumbwa na tatizo la kupata pembejeo za kilimo.

Amiri Eliasa mkulima wa tumbaku kutoka Urambo mkoani Tabora amesema Serikali inapaswa kushuka chini ili kuweza kuwafikia wakulima ambao wapo maeneo ya vijijini na wamekuwa wakitumia gharama kubwa kufuatilia ruzuku ya mbolea ambayo imekuwa ikitolewa mijini na siyo vijijini ambako kuna wakulima wengi.

Eliasa anasema Ruzuku tumejiandikisha vijijini lakini cha ajabu ruzuku hii tunakwenda kuichukulia mjini tena kwa matajiri ikafikia hatua ya mwisho ruzuku inanunuliwa na matajiri wakiwa na namba zile za ruzuku za wakulima na baadae wakulima tunakwenda kununua tena kwa matajiri serikali ishuke chini.

Mashamba ya pamoja huko Chinangali Dodoma, Tanzania.
Mashamba ya pamoja huko Chinangali Dodoma, Tanzania.

Aidha bajeti ya wizara ya kilimo kwa mwaka 2023/24 inakadiriwa kuwa na ongezeko la asilimia 29.24 ambayo ni sawa na shilingi bilioni 970.78 ikilinganishwa na bajeti iliyopita ambayo ilikuwa ni shilingi bilioni 751.12 hali iliyoleta matumaini kwa wataalamu wa kilimo wakisema bajeti hiyo itakwenda kulenga maeneo ya utafiti wenye tija,uzalishaji wa mbegu bora ambayo ndio misingi ya ukuaji wa kilimo.

Mmoja wa wataalamu hao Dkt Eliaza Mkuna ambaye ni msimamizi katika idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Mzumbe amesema kuboreshwa kwa huduma za upatikanaji wa mbegu bora kutapelekea kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji wenye tija.

Dkt Mkuna anaeleza kuwa ilivyokuwa sio lazima mkulima kule chini afuatwe kabisa apewe kila kitu aambiwe mpaka na pesa zako hizi hapa lakini hizi huduma zikiboreshwa kwa mfano kukapatikana mbegu bora inamaanisha kwamba huyu mkulima hata akienda kwenye soko lolote akiweza kununua mbegu zake ana uhakika wa kuvuna na ikamsaidia kwenye chakula na kipato chake.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akizungumza na waandishi wa habari. Picha kwa hisani ya Ikulu, Dar es Salaam, Tanzania
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akizungumza na waandishi wa habari. Picha kwa hisani ya Ikulu, Dar es Salaam, Tanzania

Hata hivyo Mhandisi Octavian Lasway Mkurungezi wa kampuni ya Holly Green inayo jishughulisha na masuala ya kilimo mkoani Morogoro amesema licha ya bajeti iliyopita ya mwaka 2022/23 kutengewa fedha nyingi bado kumekuwa na changamoto katika utoaji wa fedha kwa ajili ya bajeti hizo kwani kuna baadhi ya malengo yaliyowekwa katika bajeti iliyopita hayakufikiwa.

Mhandisi Lasway anasema kwenye utekelezaji wake kuna malengo ambayo yamefikiwa na malengo ambayo hayakufikiwa kutokana na uhaba au ukosefu wa pesa ambazo zilitengwa kwa sababu kutenga bajeti ni kitu kimoja lakini kutoa hela kwa ajili ya bajeti ile kwenye utekelezaji ni kitu kingine.

Mhandisi Lasway ameishauri serikali kuendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya umwagiliaji na matumizi ya sayansi na teknolojia katika kilimo ili kuweza kufikia malengo ya kuweza kuzalisha chakula cha kutosha kwa Afrika na dunia nzima kwa ujumla.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Dar es Salaam

XS
SM
MD
LG