Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 12:49

Ruto na Samia waahidi kuboresha maslahi ya wafanyakazi


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiagana na mgeni wake rais wa Kenya Dkt. William Ruto mara baada ya kuhitimisha ziara yake jijini Dar es Salaam tarehe 10, Oktoba 2022. Picha kwa Hisani ya Ikulu, Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiagana na mgeni wake rais wa Kenya Dkt. William Ruto mara baada ya kuhitimisha ziara yake jijini Dar es Salaam tarehe 10, Oktoba 2022. Picha kwa Hisani ya Ikulu, Dar es Salaam.

Rais wa Kenya, William Ruto Jumatatu aliongoza sherehe za siku ya wafanyakazi duniani katika bustani ya Uhuru iliyoko katika jiji la Nairobi. Wakati wa maadhimisho hayo, Ruto alichukua nafasi kufafanua mikakati iliyowekwa na serikali yake katika kusaidia baadhi ya sekta zinazokua nchini nchini humo.

Katika sekta ya kilimo rais huyo alitangaza kuwa serikali yake itatoa bajeti kubwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya masoko katika kila eneo la bunge nchini Kenya, kuongeza nafasi za kazi 2,000 kila mwaka pamoja na kuanzisha mpango wa ulipaji fidia kwa wafanyakazi wanaojeruhiwa kazini.

Maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi nchini Kenya yamekuja wakati hali ya kisiasa nchini humo inayumba kutokana na azma ya muungano wa upinzani wa Azimio wa kuanzisha tena maandamano ya kila wiki ambayo yametishia ajenda ya serikali ya kuimarisha uchumi.

Aidha Rais William Ruto ameutaka Muungano wa Azimio kuepuka ghasia na uharibifu wa mali, huku akilitaka kundi linayoongozwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuzingatia mazungumzo ya pande mbili bungeni.

Ruto alisema kuwa ni wajibu wake kama rais kulinda haki na mali za Wakenya wote, na kuongeza kuwa “hataruhusu uharibifu wa mali”.

Madhimisho ya siku ya wafanyakazi pia yamekuja wakati ambapo Serikali ya Kenya inakabiliwa na mgogoro wa kifedha ambao haujawahi kutokea uliosababisha ucheleweshwaji wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma na wafanyikazi wa kaunti.

Mwandamanaji wakati wa maandamano ya Mei Mosi huko Nairobi tarehe 1, Mei 2021. Picha na Ed Ram / AFP.
Mwandamanaji wakati wa maandamano ya Mei Mosi huko Nairobi tarehe 1, Mei 2021. Picha na Ed Ram / AFP.

Nchini Tanzania wafanyakazi wameahidiwa kurejeshewa mfumo wa nyongeza ya mishahara wa kila mwaka ambayo ilikuwa umesitishwa miaka saba iliyopita na aliyekuwa raisi wa awamu ya tano John Pombe magufuli.

Wafanyakazi hao pia wameitaka serikali kusimamia utekelezaji wa sheria za kazi ili kuleta usawa na haki katika maeneo ya kazi na kuepuka na tabia yakuongeza mishahara kama hisani

Maadhimisho hayo ya siku ya wafanyakazi yalifanyika katika mkoa wa Morogoro, Rais Samia Suluhu Hassan amewaahidi wafanyakazi kuondoa kizuizi hicho ambacho kilidaiwa na wafanyakazi kupunguza motisha wa uwajibikaji kazini suala ambalo limechangia sheria za kazi kuozingatiwa.

Mwalimu Philbert Macheyeki mkazi wa mkoa wa Mwanza alisema suala la nyongeza ya mishahara ni la kisheria na sio hisani ya Rais, licha ya kuondolewa na uongozi uliopita.

“Mishahara na masilahi na marupurupu ya kazi ikiwepo ya uwalimu yanapaswa yalindwe na sheria na wala siyo kuchukuliwa kama hisani ya viongozi waliopo madarakani. Sheria ya kazi inasema kwamba mfanyakazi yeyote aidha wa sekta binafsi au ya umma ni lazima aongezewe mshahara wake kila baada ya muda fulani. Sheria iko wazi.” Alisema Macheyeki.

Aidha rais Samia alitoa ufafanuzi kuhusu asilimia 23.3 ya mshahara ambayo serikali ilipandisha mwaka jana kuwa kiwango hicho hakikuweza kumnufaisha kila mfanyakazi mbali na kuwa lengo la nyongeza hiyo ni kuwainua wafanyakazi wa kima cha chini, lakini wengi wao hawakunufaika.

Wakati watumishi wa umma wametangaziwa nyongeza ya mishahara, wastaafu pia wameitaka serikali kuwatengenezea mazingira mazuri na rahisi yatakayowawezesha kufurahia maisha ya ustaafu kwa kuwawekea mifumo rafiki na kuwapunguzia kero la kusafiri umbali mrefu ili kuhakiki taarifa zao, na wamelitaka shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini kutoa elimu zaidi kuhusu malipo ya pensheni kwa wastaafu hao.

Hata hivyo shirikisho hilo la vyama vya wafanyakazi Tanzania TUCTA limesema kukosekana kwa mifumo imara ya hifadhi ya jamii kunaongeza changamoto kwa wastaafu wanapotakiwa kwenda kuhakiki taarifa zao, hali ambayo huwafanya wastaafu kutumia gharama kubwa kitu ambachi husababisha kupoteza haki zao kwa kushidwa kuthibitisha taarifa zao kutoakana na kushindwa kugharamia safari wakati wengine wakisumbuliwa na maradhi.

XS
SM
MD
LG