Maadhimisho yamegubikwa na wito wa wafanyakazi kutaka nyongeza ya mishahara, kupunguziwa masaa ya kufanya kazi na kuboreshwa mazingira ya kazi.
Zaidi ya watu 100,000 wamejitokeza katika sehemu mbali mbali za Korea Kusini kwa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, ikiwa ni maadhimisho makubwa kuwahi kufanyika tangu kuanza kwa janga la virusi vya Corona mapema mwaka 2020.
Mikutano mikubwa miwili imefanyika mjini Seoul, kila mkutano ukihudhuriwa na watu 30,000.
Mjini Taipei nchini Taiwana, makundi ya kutetea haki za wafanyakazi yamepeperusha bendera zinazowakilisha miungano yao ya wafanyakazi.
Baadhi ya wafanyakazi wa afya walivalia mavazi ya kazi na kubeba mabango yenye ujumbe unaoitaka serikali kuweka ruzuku kwa bidhaa muhimu, na wengine wakibeba mabango yanayokosoa sera za kikazi za rais Tsai Ing Wen na kuongeza shinkizo dhidi ya chama kinachotawala kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2024.