Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 00:57

Vita vyapamba moto Khartoum


Moshi ukifuka juu ya majengo kusini mwa jiji la Khartoum, wakati mapigano yakiendelea Mei 16 2023. Picha na AFP.
Moshi ukifuka juu ya majengo kusini mwa jiji la Khartoum, wakati mapigano yakiendelea Mei 16 2023. Picha na AFP.

Mashambulizi ya anga na mizinga yameongezeka kwa kasi katika mji mkuu wa Sudan siku ya Jumanne asubuhi, wakaazi wa mji huo walisema, wakati jeshi likijaribu kulinda kambi muhimu kutoka kwa wapinzani wa kijeshi ambao wamekuwa wakipambana nao kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Mashambulizi ya anga, milipuko na mapigano yaliweza kusikika kusini mwa mji wa Khartoum, na kulikuwa na mashambulizi makali ya makombora katika maeneo mbali mbali ya mto Nile yanayopakana na miji ya Bahri na Omdurman, mashuhuda walisema.

Mapigano kati ya jeshi na vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) yamesababisha machafuko katika maeneo mengine ya Sudan, hususani katika eneo la Darfur Magharibi, lakini mapigano zaidi yako katika jiji la Khartoum.

Mzozo huo umesababisha mgogoro wa kibinadamu ambao unatishia ukosefu wa utulivu katika eneo hilo, ambapo zaidi ya watu 700,000 wamekoseshwa makazi nchini Sudan na wengine takriban 200,000 kulazimika kukimbilia nchi jirani.

Wale ambao wamebaki katika mji mkuu wanahangaika kujikimu kimaisha kadiri upatikanaji wa chakula unavyopungua, huduma za afya zikiporomoka na uasi kuenea.

Maafisa wamerekodi vifo vya watu 676 na zaidi ya 5,500 kujeruhiwa. Lakini idadi halisi inatarajiwa kuwa kubwa zaidi wakati taarifa nyingi zinaeleza kuwa miili ya watu imeachwa barabarani na watu kuhangaika jinsi ya kuwazika marehemu.

"Hali haivumiliki. Tuliondoka nyumbani kwetu kwenda kwenye nyumba ya jirani katika mji wa Khartoum, tulikuwa tukitoroka vita, lakini mashambulizi ya mabomu yanatufuata popote tunapokwenda," alisema Ayman Hassan, mkazi wa eneo hilo mwenye umri wa miaka 32. "Hatujui wananchi walifanya nini kustahili vita katikati ya majumba."

Mapigano yameongezeka Khartoum na Geneina, mji mkuu wa Darfur Magharibi, tangu pande hizo mbili zilizohasimiana zilipoanza mazungumzo mjini Jeddah, yaliyosimamiwa na Saudi Arabia na Marekani zaidi ya wiki moja iliyopita.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters.

XS
SM
MD
LG