Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 08:33

UN : Mataifa ya nje yamepindukia mipaka kujihusisha na mgogoro wa Libya


Mzee nchini Libya akishiriki katika maandamano katika uwanja wa mashahidi wa vita mjini Tripoli, eneo linaloshikiliwa na Serikali ya umoja wa kitaifa (GNA) inatambuliwa na UN, Juni 21, 2020.
Mzee nchini Libya akishiriki katika maandamano katika uwanja wa mashahidi wa vita mjini Tripoli, eneo linaloshikiliwa na Serikali ya umoja wa kitaifa (GNA) inatambuliwa na UN, Juni 21, 2020.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres amelionya baraza la usalama kwamba mzozo wa Libya umeingia katika awamu mpya ambapo uingiliaji kati wa kigeni umefikia viwango ambavyo havijapata kushuhudiwa. 

\Wakati huo huo vyombo vya habari vinaripoti kwamba wapiganaji wa pande mbili nchini humo wako katika mapigano mapya kati ya miji ya Misrata na Sirte.

Akizungumza kwenye kikao cha baraza la usalama Jumatano kilichohudhuriwa pia na mawaziri wa mambo ya nje kwa njia ya video, katibu mkuu Gutterres, amesema hakuna tena muda huko Libya, ambako uingiliaji kati kutoka nchi za nje umeongezeka kwa hali ya juu pamoja na kupelekwa kwa vifaa na silaha za kisasa pamoja na mamluki wanaoongezeka.

Katibu mkuu anasema:“Tuna wasi wasi mkubwa sana kutokana na kiwango cha kuimarishwa shughuli za kijeshi karibu na mji wa Sirte na kiwango cha juu cha uingiliaji kati kutoka nchi za nje katika mzozo huu, kwa kukiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa na ahadi zilizotolewa Berlin na mataifa wanachama wa baraza hili la usalama.”

Gutterres ameendelea kusema kwamba licha ya kuongezeka kwa mivutano UN imeendelea kujadiliana na pande zote ili kuzuia vita kuenea katika jimbo lenye utajiri wa mafuta ambalo linazalisha asilimia 60 ya mapato ya mafuta ya nchi hiyo.

Wapiganaji wa serikali ya GNA inayotambuliwa na UN walionekana wakitayarisha silaha zao kabla ya kuelekea mji wa Sirte kutokea magharibi huku wapiganaji wa mashariki wakijitayarisha pia.

Mji huo umegeuka haraka kuwa mstari wa mbele katika vita hivyo baada ya wanajeshi wa serikali ya Tripoli wakisaidiwa na Uturuki kuwarudisha nyuma wapiganaji wa jeshi la taifa la Libya LNA kutoka Tripoli na maeneo ya kaskazini magharibi ambako wamekuwepo tangu mwezi April 2019.

Jeshi la LNA linaloongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar linaloungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu, Russia na Misri limepatwa na pigo kubwa mnamo wiki mbili ziliopita kwa kurudishwa nyuma hadi mji huo wa Sirte. Jeshi la serikali lilizuiliwa karibu na Sirte kutokana na mashambulizi ya ndege zisizojulikana zimeokea wapi mwishoni mwa wiki iliyopita.

Msemaji wa jeshi la serikali, Mohamed Qanunu, alisema mapema wiki hii kwamba wao hawapendelei vita.

Mohameds Qanunu, msemaji wa serikali ya GNA anasema:

“Sisi hatukuanzisha vita. Sisi hatuanzishi vita kwa vile tunapenda kuuwa au kuuliwa, lakini tunabidi kupigana ili kukomboa miji kutoka kwa wanamgambo na makundi ya uhalifu. Ikiwa hili linaweza kufanyika kwa amani sisi tuko tayari.”

Serikali ya Tripoli inaungwa mkono na Qatar, Italy na Uturuki.

Juhudi kubwa za kidiplomasia zinaendelea kati ya mataifa yanaohusika katika vita hivyo ili kutafuta njia za kumaliza mzozo kwa mazungumzo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas kwa pande wake anatoa wito wa majadiliano kuanza tena.

Heiko Maas, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani anasema:

“Itakuwa jambo zuri ikiwa matatizo yaliyopo yanaweza kutanzuliwa kwa majadiliano, na hilo linaweza kufanyika kwa njia ya mazungumzo ya dhati, wazi, na tunatumaini jambo hilo litafanyika katika siku chache zijazo.”

Mwishoni mwa wiki wakazi wa mji wa Benghazi waliandamana dhidi ya uingiliaji kati wa Uturuki katika mambo ya ndani ya nchi yao.

Libya imekuwa katika hali ya ghasia tangu 2011 baada ya kupinduliwa kwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Ghaddafi na tangu 2015 imegawika kati ya serikali ya GNA na LNA ya mashariki.

Juhudi za UN kutafuta suluhisho la amani hadi hivi sasa hazijafanikiwa na wachambuzi wanasema njia pekee ni kwa Uturuki na Rashia kufikia makubaliano kumaliza mzozo huo wa Libya.

Imetayarishwa na Mwandishi ketu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG