Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:36

Uganda yatishia kuingia DRC


Rais Joseph Kabila
Rais Joseph Kabila

Serikali ya Uganda imetishia kuwafuata hadi ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, watu wanaowashambulia raia wake katika eneo la Ziwa Albert.

Waziri wa masuala ya kikanda wa Uganda Philemon Mateke, ameiambia Sauti ya Amerika kwa mahojiano ya simu kwamba Uganda imefikia hatua ya kutovumilia tena kile ametaja kama uchokozi kutoka kwa watu wa DRC, wanaoingia Uganda na kuwapiga, kuwauwa na kuwajeruhi raia wake hasa katika ziwa Albert.

“Tunawaomba Wakongo, waache kutuchokoza. Tumekuwa wenye ustaarab kwa mda mrefu. Kazi yetu kama serikali ni kuwalinda raia na mali yao” amesema Waziri Mateke.

Mateke amesema Serikali ya Uganda imekuwa ikitumia mbinu za kidiplomasia kusuluhisha migogoro kati yake na DRC, ikiwemo suala la kukabiliana na waasi wa Allied Democratic Forces, ADF, lakini sasa mashambulizi kutoka DRC yamezidi na kwamba Uganda ipo tayari kujibu mashambulizi hayo kwa nguvu za kijeshi.

“Wakiendelea kutuchokoza, tutajibu. Tunachoka. Hatuna uvumilivu tena. Sehemu wanakotoka watu hawa hakuna uongozi thabithi. Kwa hivyo, hatuna watu wa kuzungumza nao kumaliza mashambulizi yao. Hata jana Jumanne wameuwa watu 12 katika eneo la Ziwa Albert,” ameendelea kusema waziri Mateke.

Juhudi za kuwapata maafisa wa DRC kujibu tuhuma hizi kwa njia ya simu hazikufaulu.

Waziri Mateke ametaja kundi la ADF kuwa kundi sumbufu lakini hatari, ambalo serikali ya Uganda ilikuwa karibu inalishinda nguvu kabla ya serikali ya DRC kuwazuia wanajeshi wa Uganda na sasa kundi hilo limegeuka tena kuwa hatari kwa DRC na majirani zake, akiongezea kwamba muda utafika, watakabiliana nao vilivyo.

Msemaji wa Jeshi la Uganda, UPDF, Brigedia Richard Karemere, ameiambia VOA kwamba wana taarifa kwamba wanao tekeleza mashambulizi dhidi ya wavuvi katika Ziwa Albert, ni maafisa wa Jeshi la Kongo kwa ushirikiano na makundi ya wapiganaji.

Keremere amesema kwamba kwa sasa wanajeshi wa Uganda wako mpakani tayari kukabiliana na kundi la ADF pamoja na kundi lolote lile linaloweza kuingia Uganda na kulezea kwamba wapo tayari kuingia DRC iwapo serikali ya Joseph Kabila itawaruhusu.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington DC

XS
SM
MD
LG