Gharama za kamera
Jumla ya dola milioni 124 zitatumika kuweka kamera za cctv 5552 katika jiji la Kampala na mji iliyo jirani, hatua ambayo Rais wa Uganda Yoweri Museveni anaamini kwamba itasaidia kuwanasa wahalifu.
Msemaji wa polisi wa Uganda Emilian Kayima amesema tayari kamera hizo zimewasili jijini Kampala baada ya kuagizwa na kampuni ya Huawei inayotengeneza na kuuza vifaa vya elektroniki.
"Kuwepo kwa kamera za cctv kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuwatambua na kuwanasa wahalifu. Tutaweka kamera za cctv 5552 kote nchini, jiji la Kampala, zipatazo kamera 3000," amesema.
Kituo maalum cha kufuatilia matokeo
Makao makuu ya kufuatilia kila linalotendeka nchini Uganda, jinsi yatakavyonaswa na kamera hizo, yanajengwa katika makao makuu ya polisi, katika mtaa wa Naguru, jijini Kampala, na kuanza kutumika mwezi Julai 2019.
Msemaji wa polisi Kayima, ameeleza kwamba hadi sasa, camera hizo zimewekwa kwenye barabara kuu, umbali wa kilomita 20 kutoka jijini kampala, katika maeneo ya siri.
Hatua ya kuweka kamera katika jiji la Kampala na maeneo mengine ya Uganda, inajiri baada ya kuuwawa kwa aliyekuwa msemaji wa polisi Felix Kaweesi na mbunge wa manispaa ya Arua Ibrahim Abiriga.
Rais Museveni
Rais Museveni aliamrisha kuwekwa kwa kamera hizo na bunge lilipitisha bajeti ya dola milioni 61 kufanikisha mradi huo.
Polisi wanasema kwamba kamera hizo zitawasaidia sana kutokana na idadi ndogo ya maafisa wa polisi.
Uganda iliwahi kuweka kamera za cctv kwenye barabara kuu ya kutoka uwanja wa ndege wa Entebbe hadi kati kati mwa jiji la Kampala, wakati wa mkutano wa jumuiya ya madola - CHOGM - mnamo mwaka 2007, lakini mwaka mmoja baada ya mkutano huo, kamera hizo ziliripotiwa kutofanya kazi.
Serikali Kuimarisha ulinzi
Mbali na kuweka kamera za cctv, museveni anataka waendesha pikipiki maarufu kama boda boda, kupewa nambari maalum, wanaovaa fulana zinazofunika nyuso zao kukamatwa, magari kuweka vifaa maalum vya elektroniki ili kuweza kufuatiliwa kila yanapokwenda, miongoni mwa mengine.
Katika matukio yote vya mauaji kwa kupigwa risasi ambayo yameripotiwa nchini Uganda ikiwemo mauaji ya mashehe, msemaji wa polisi Felix Kaweezi, Mbunge Ibrahim Abiriga, wanawake kadhaa na utekaji nyara, hakuna aliyewahi kufikishwa mahakamani na kupatikana ushahidi wa kutosha.
Idadi kubwa ya vifo imekuwa ikihusishwa na kundi la Allied democratic forces ADF.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington, DC