Watu takribani 50 waliuwawa na wengine 100 walipata majeraha mabaya ya kuungua moto baada ya lori la mafuta kugongana na gari moja huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC siku ya Jumamosi ofisa wa jimbo la Kongo Central alisema.
Naibu gavana wa jimbo, Atou Matubuana Nkuluki alisema maafisa katika eneo hilo walifanya kila wawezalo kuwasaidia waathirika kwenye ajali hiyo iliyotokea katika kijiji cha Mbuta kiasi cha kilomita 130 kutoka mji mkuu wa DRC, Kinshasa.
Nkuluki alisema "tunaomboleza vifo vya takribani watu 50. Pia kuna watu wengine 100 ambao wamepata majeraha ya moto". Aliongeza kusema kwamba barabara katika taifa hilo lililopo Afrika ya kati ni mbaya baada ya miaka kadhaa ya vita na kutelekezwa bila ukarabati.
Mwaka 2010 watu takribani 230 waliuwawa huko Congo wakati lori la mafuta lilipopinduka na kulipuka na kusababisha moto kuwaka hadi kufikia nyumba kadhaa pamoja na ukumbi wa sinema uliojaa watu waliokuwa wakiangalia michuano ya kombe la dunia.