Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 16:29

Uganda: Lori lililoegeshwa bila alama za hatari lasababisha vifo vya abiria 16


Mji wa Kampala, Uganda
Mji wa Kampala, Uganda

Watu wasiopungua 16 wamefariki na wengine 21 kujeruhiwa baada ya basi lililokuwa linaelekea Gulu kuligonga lori ambalo limeegeshwa katika kituo cha biashara cha Adebe huko Kamdini kwenye  barabara kuu ya Kampala -Gulu kaskazini mwa Uganda Ijumaa.

Polisi walisema watu 12 walifariki hapo hapo, wakati wengine wanne walifariki kwenye hospitali ya Atapara ambako walikimbizwa kupatiwa matibabu.

“Inadaiwa kuwa basi lenye namba za usajili UAT 259P, ambalo linamilikiwa na kampuni ya Roblyn, lilikuwa likitoka Kampala kwenda Gulu lilipoligonga lori majira ya saa sita usiku Januari 6, 2023 katika barabara kuu ya Kampala-Gulu. Lori hilo linadaiwa kuwa lilikuwa likipakia mizigo katika kituo cha biashara cha Adebe kilichopo kilomita moja kufika sehemu ya ukaguzi ya Kamdini,” msemaji wa polisi wa mkoa wa North Kyoga Patrick Jimmy alisema.

Watu waliofariki katika walipelekwa katika kituo cha afya cha Anyeke kufanyiwa uchunguzi, aliongeza kusema.

“Sababu ya ajali hiyo bado haijajulikana, lakini taarifa za awali zinaonyesha ni uegeshaji mbaya uliofanywa na dereva wa lori bila ya kuweka alama za hatari. Ni tukio la kusikitisha sana. Tunatoa wito wa utulivu kutoka kwa umma; na tunawapa pole familia zilizofikwa na msiba huu,” alisema.

Uganda imeshuhudia ongezeko la ajali za barabarani katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuu.

Siku ya Jumanne, polisi wa barabarani walieleza kuwa idadi ya ajali za barabarani 104 zilisajiliwa nchi nzima kati ya Desemba 30, 2022 na Januari 1.

Ripoti iliyotolewa na msemaji wa polisi wa barabarani, mrakibu msaidizi wa polisi Faridah Nampiima, ilionyesha kuwa ajali 28 kati ya hizo zilipelekea watu kupoteza maisha.

“…ajali 49 zilikuwa mbaya sana na 27 zilikuwa ndogo kuanzia Desemba 30, 2022 hadi Januari 1. Kati ya ajali za barabarani 104, tulisajili waathirika 149, 35 walifariki na 114 walijeruhiwa vibaya sana,” alisema.

Kulingana na polisi, sababu kubwa kabisa ya ajali za barabarani ni uendeshaji mbaya wa magari.

Chanzo cha habari hii kinatokana na gazeti la "The East African".

XS
SM
MD
LG