Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 08:17

Mtoto wa Museveni anaunga mkono M23, ndege za kurusha makombora zimewasili Goma


Waasi wa M23 wakitembea katika mji wa Karuba, kilomita 62 kutoka Goma, Kivu kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Waasi wa M23 wakitembea katika mji wa Karuba, kilomita 62 kutoka Goma, Kivu kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Mtoto wa rais wa Uganda Yoweri Museveni, Lt. Jenerali Muhoozi Kainerugaba, amesema kwamba kundi la waasi la M23, linalopigana vita na jeshi la serikali ya Kinshasa, lina haki ya kufanya hivyo.

Muhoozi ameandika ujumbe wa twiter akisema kwamba “ni hatari sana kwa mtu yeyote kupiga vita ndugu zetu. Sio magaidi, wanapigania haki za Watutsi wanaoishi DRC.”

Msimamo wa Generali Muhoozi ni tofauti na msimamo wa serikali ya Uganda ambayo imelazimika kutoa taarifa kupitia kwa msemaji wake Ofwono Opondo, kufuatia ripoti kwamba Uganda inaunga mkono wapiganaji wa M23.

Opondo alisema wiki hii kwamba “Uganda haiungi mkono kundi la waasi la M23” na kwamba “Uganda ina husiano mzuri sana na serikali ya Kinshasa katika kupigana na kundi la waasi la Allied democratic movement ADF.”

Raia wa DRC waliandamana mapema wiki hii, hadi kwenye mpaka wa DRC na Rwanda, wakidai kwamba Uganda na Rwanda wanaunga mkono waasi wa M23, na kutaka mpaka kati ya DRC na nchi hizo mbili kufungwa.

Baadhi wa bunge na maseneta wa DRC vile vile walitaka DRC kufunga mpaka wake na Uganda, wakisema kwamba Uganda inaunga mkono makundi ya wapiganaji wanaoisumbua serikali ya Congo.

Akikutana na wajumbe wa umoja wa ulaya katika makao makuu ya jeshi la Uganda, Mbuya, karibu na Kampala, Alhamisi wiki hii, naibu kamanda wa jeshi la Uganda Generali Peter Elwelu, alisema kwamba “kundi la M23 linastahili kurudi katika sehemu zake ambazo lilikuwa linashikilia ili kuruhusu mazungumzo kufanyika.”

Ndege za kijeshi zimewasili Goma

Kenya imetangaza kwamba jeshi lake lipo tayari kuingia mashariki mwa DRC kwa ajili ya kupambana na makundi ya waasi.

Wanajeshi wa Burundi tayari wapo DRC kupambana na kundi la waasi la Red Tabara.

Uganda inapambana na kundi la waasi la ADF.

Lt. Gen. Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa rais wa Uganda Yoweri Museveni May 7, 2022.
Lt. Gen. Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa rais wa Uganda Yoweri Museveni May 7, 2022.

Mapema leo Jumapili, ndege za vita za DRC zimewasili mjini Goma. Japo serikali haijatoa taarifa yoyote kuhusu ndege zake za kurusha makombora na zile zisizo na rubani kuwasili Goma, vyombo vya habari vya DRC vimeripoti kwamba jeshi la DRC lipo tayari kuanza mashambulizi makali dhidi ya makundi ya waasi mashariki mwa nchi hiyo.

Usafiri wa ndege za kawaida umesitishwa kwa saa kadhaa wakati ndege hizo za kijeshi zilikuwa zinaingia Goma.

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imedai kwamba waasi wa M23 wanasaidiwa na serikali ya Rwanda, madai ambayo serikali ya Rwanda imekuwa ikikana kila mara.

M23 wanadai kulinda maslahi ya watu wanaozungumza Kinyarwanda

Waasi wa M23 wamesema kwamba wanalinda maslahi ya watu wanaozungumza Kinyarwanda, wanaoishi katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, dhidi ya kundi la waasi la FDLR, ambalo linashutumiwa kwa mauaji ya kimbari yam waka 1994.

Serikali ya Congo na makundi ya kutetea haki za kibinadamu, yanashutumu kundi la M23 kwa ukandamizaji wa haki za kibinadamu, na kudaiwa kuwa sehemu ya jeshi la Rwanda.

Kundi la M23 limedhibiti mji wa Bunagana na kuathiri Maisha ya kawaida ya karibu watu 200,000, ambao wamekimbilia Uganda kama wakimbizi. Ujenzi wa Barabara kutoka Bunagana hadi Goma, ambao umekuwa ukitekelezwa na serikali ya Uganda pia umesitishwa.

Luteni Generali Muhoozi Kainerugaba, amekuwa akiandika ujumbe wenye utata kila mara, na mara nyingi kupelekea wachambuzi wa siasa za Afrika mashariki na maziwa makuu kusema kwamba huenda anaandika yake anayosikia kutoka kwa baadhi ya viongozi, kutokana na uhusiano wake wa karibu na rais wa Rwanda Paul Kagame, na babake Yoweri Museveni.

XS
SM
MD
LG