Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 20:00

Mtoto wa Museveni ameonya jeshi la Uganda dhidi ya kushambulia M23


Jenerali Muhoozi Kainerugaba (kushoto) akiwa na rais wa Rwanda Paul Kagame katika mikutano yao ambayo imekuwa ikifanyika kila mara mwaka huu, mjini Kigali, Rwanda
Jenerali Muhoozi Kainerugaba (kushoto) akiwa na rais wa Rwanda Paul Kagame katika mikutano yao ambayo imekuwa ikifanyika kila mara mwaka huu, mjini Kigali, Rwanda

Mtoto wa rais wa Uganda ameonya jeshi la nchi hiyo kuacha kudhihaki kundi la waasi la M23 akiwaita waasi hao kuwa ndugu zake.

Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni Jenerali katika jeshi la Uganda UPDF, ameandika ujumbe wa twiter wakati Uganda inatayarisha wanajeshi 1000 kuingia Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kupambana na kundi la waasi la M23.

Alikuwa kamanda wa kikosi cha jeshi la ardhini kinachoenda kupigana DRC, kabla ya kupandishwa cheo na kuwa Jeenerali na kuondolewa kuwa kamanda wa kikosi hicho.

Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mtoto wa rais Yoweri Museveni, amekuwa akiandika ujumbe wa twiter kuunga mkono waasi wa M23.

Ujumbe wake wa kuonya jeshi la UPDF, ambalo analitumikia, unajiri siku chache baada ya naibu wa mkuu wa jeshi la Uganda Luteni Jenerali Peter Elwelu, kusema kwamba jeshi la Jumuiya ya Afrika mashariki lina uwezo wa kusambaratisha waasi wa M23 katika muda was aa 24.

“Nilisikia baadhi ya watu wakisema kwamba wanaweza kuwashinda nguvu M23 katika muda wa siku moja? Sawa, hivyo ndivyo Obote alikuwa akisema kuhusu NRA wakiwa Luweero,” ameandika Muhoozi.

Milton Obote, alikuwa rais wa Uganda wakati Yoweri Museveni na waasi wake wa National resistance Army NRA walikuwa Luweero, wakipigana kuelekea Kampala. Museveni na waasi wa NRA walipigana na kupindua serikali. Amekuwa madarakani tangu mwaka 1986.

Muhoozi ameendelea kusema kwamba waasi wa M23 wanastahili “kubembelezwa ili kuacha kupigana kwa ajili ya amani na kwamba watakubali hatua hiyo kwa sababu wanapenda DRC iwe na amani.”

Mapema mwezi uliopita, Muhoozi Kainerugaba aliandika ujumbe kuunga mkono waasi wa M23, akisema kwamba “uasi wao ni wa haki.”

“Ni hatari sana kwa mtu yeyote kupigana na hao ndugu wetu. Sio magaidi! Wanapigania haki za Watutsi wanaoishi DRC,” aliandika Muhoozi kwenye twiter.

Mazungumzo ya amani DRC

Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi (Kulia) akiwa na rais wa Kenya William Ruto mjini Kinshasa, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi (Kulia) akiwa na rais wa Kenya William Ruto mjini Kinshasa, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Rais wa Kenya Dr. William Ruto amekuwa Kinshasa kwa mazungumzo ya amani nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Ruto amesisitiza kwamba Kenya imejitolea kuhakikisha kwamba kuna usalama mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Mkutano huo pia uliangazia ushirikiano mpana kati ya Kneya na DR Congo ambapo zaidi ya makundi ya waasi 120 yanayopigana na wanajeshi wa serikali, tisho kubwa likiwa kundi la M23.

Kenya imetuma karibu wanajeshi 900 kulinda usalama mashariki mwa DRC kufuatia makubaliano ya viongozi wa jumuiya ya Afrika mashariki, kuunda jeshi la pamoja kupambana na waasi masharii mwa Kivu kaskazini, Kuini na Ituri. Jeshi hilo litaongozwa na kamanda kutoka Kenya.

Mkutano kuhusu mazungumzo ya kutafuta amani mashariki mwa DRC ulikuwa umepangiwa kuwanyika hii leo mjini Nairobi, Kenya, lakini umeahirishwa bila taarifa kamili kutolewa.

Jeshi la umoja wa mataifa limekuwa DRC kwa miaka mingi kwa ajili ya kulinda amani, lakini limekosolewa kwa kutofanya ya kutosha kumaliza mashambulizi ya waasi.

Ruto amesema kwamba jukumu la kikosi cha jeshi la Afrika mashariki yamekubaliwa na viongozi wote wa Jumuiya, na umoja wa Afrika pamoja na baraza la usalama la umoja wa mataifa limefahamishwa.

Uganda inatuma wanajeshi kupambana na M23 huku ikiendelea kupambana na ADF

Serikali ya Uganda imesema kwamba itatuma wanajeshi wake 1000 katika nchi Jirani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kufikia mwishoni mwa mwezi huu.

Wanajeshi hao wanaingia mashariki mwa DRC chini ya makubaliano ya Jumuiya ya Afrika mashariki.

Nchi saba za jumuiya ya Afrika mashariki zilikubaliana kutuma wanajeshi kupambana na makundi ya waasi ambayo yamesababisha ukosefu wa usalama mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kwa miongo kadhaa.

Uganda itakuwa nchi ya tatu kutuma wanajeshi wake nchini Congo baada ya Kenya na Burundi.

Msemaji wa jeshi la Uganda Brigendia Jenerali Felix Kulaigye amesema kwamba wanajeshi wa Uganda wapo tayari kusaidia katika kurejesha amani katika nchi hiyo Jirani.

Wanajeshi wa Uganda wakiwa pamoja na wanajeshi wa DRC katika oparesheni dhidi ya waasi wa Allied democratic forces ADF
Wanajeshi wa Uganda wakiwa pamoja na wanajeshi wa DRC katika oparesheni dhidi ya waasi wa Allied democratic forces ADF

Uganda na Rwanda zinadaiwa kuunga mkono M23

Hata hivyo, baadhi ya makundi ya kijamii yamekuwa yakidai kwamba Uganda inahusika pakubwa na vita vianvyoendelea Congo, yakidai kwamba inaunga mkono waasi wa M23.

Tayari Uganda ina wanajeshi wake nchini DRC, wanaopigana na kundi la waasi la Allied democratic Forces ADF.

Uganda imelipa DRC dola milioni 65 kama sehemu yad ola milioni 325 ilizoagizwa kulipa Congo kwa hasara ambayo Congo ilipata wakati wanajeshi wa Uganda waliingia nchini humo miaka ya 1990.

Licha ya mabilioni ya dola kutumika kwa kikosi cha jeshi la umoja wa mataifa kulinda amani nchini DRC, bado kuna zaidi ya makundi ya waasi 120 likiwemo kundi la M23, yanayopigana na wanajeshi wa serikali.

DRC imeshutumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23, madai ambayo Rwanda imekuwa ikikana kila mara.

XS
SM
MD
LG