Rais aliyasema hayo siku moja tu baada ya picha zilizochapishwa katika vyombo vya habari vya Marekani kuonyesha hali mbaya inayowakabili wahamiaji, hususan watoto kwenye vituo maalum vya kuwashikilia huko Texas.
Rais Trump alituma ujumbe wa Tweet kwamba kama wahamiaji wasio na vibali hawana furaha na hali iliyopo katika vituo vilivyojengwa haraka haraka kukabiliana na hali hiyo kwa ajili yao, waambiwe wasije nchini Marekani.
Trump alisema kuwa tayari matatizo yote yametatuliwa. Pia Rais amesema tatizo hilo limesababishwa na kile alichokiita “sheria mbaya za uhamiaji za wademokrat”.
Wakati huo huo Seneta Chuck Schumer, M-democrat mwenye cheo cha juu katika baraza la Seneti alipendekeza kwamba Trump anahitaji kusoma shairi lililoandikwa juu ya Mnara wa uhuru wa new York City ambapo baadhi ya maneno yanasomeka, “nipe uchovu wako, na umaskini wako...”
Schumer alijibu ujumbe wa Trump uliokuwa katika mtandao akieleza kwamba hawa ni binadamu. Wanaokuja Marekani kutafuta maisha bora. Hivi sasa ni wakati ambapo anatakiwa akumbuke Marekani inasimamia jambo gani.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC