Huu ni mzozo kati ya Trump na Wademokrats juu ya matakwa yake ya kuwa fedha zitengwe kugharamia ujenzi wa ukuta kwenye mpaka kati ya Marekani na Mexico.
Kiongozi wa walio wengi katika baraza la Senate, Mitch McConnell anatazamiwa kuhudhuria kikao hicho, lakini haijafahamika wazi bado ikiwa kiongozi wa Wademokrat kwenye Baraza la Seneti Chuck Shumer na spika mtarajiwa wa baraza la wawakilishi Nancy Pelosi, watahudhuria kikao hicho.
Pia hajiafahamika iwapo pande zote mbili zitatumia fursa hiyo kujadili mipango ya kufungua tena shughuli za serikali baada ya kufungwa kwa siku 12 hadi Jumatano.
Wademokrats watakuwa ni walio wengi kwenye baraza la wawakilishi litakapofungua kikao chake Alhamisi, Nancy Pelosi atakaye kuwa bila shaka spika wa bunge hilo anapanga kupitisha muswada wa sheria utakao toa pesa kwa idara kadha zilizofungwa kutokana na sera za Rais Trump.
Lakini muswada wa kufadhili ujenzi wa ukuta kwenye mpaka kati ya Marekani na Mexico kwa kitita cha dola billioni 5 kama inavyopendekezwa na Rais Trump haupo kwenye ajenda ya kikao hicho cha baraza la wawakilishi cha Alhamisi.