Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 17:57

Trump : China inataka kurejea katika mazungumzo


Rais Donald Trump akiwa Ufaransa baada ya mkutano wa G7, Agosti 26, 2019. (AP Photo/Andrew Harnik)
Rais Donald Trump akiwa Ufaransa baada ya mkutano wa G7, Agosti 26, 2019. (AP Photo/Andrew Harnik)

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Jumatatu kuwa China imefunguka kwa kutaka kurejea katika mazungumzo ya kibiashara, hatua iliyokuja baada ya mataifa hayo mawili kutangaza kulipiziana kisasi hivi karibuni kwa kuongezeana kodi baina yao.

Akizungumza katika mkutano wa nchi saba matajiri zaidi G-7 huko Ufaransa, Trump aliwaambia waandishi wa habari kuwa China iliwasiliana na wawakilishi wa biashara wa ngazi ya juu wa Marekani “na kutaka warudi katika meza ya mazungumzo.”

Amesema utayari huo wa kurejea katika mazungumzo “ ni hatua nzuri sana kwa ulimwengu.”

“Wanataka mambo yafanyike. Sasa hivi, pengine hayatofanyika, lakini hii ni mara ya kwanza nimewaona kwamba wanataka kufikia makubaliano, na nafikiri ni hatua ya kutia moyo sana.”

Trump alikataa kutoa maoni yake iwapo alikuwa anawasiliana moja kwa moja na Rais wa China Xi Jinping, lakini alirejea mara kwa mara kumsifia Xi, akimwita “Kiongozi shupavu.”

Kauli ya Trump ilifuatia zile za kiongozi wa mazungumzo wa ngazi ya juu wa China Naibu Waziri Mkuu Liu He, alisema Jumatatu kuwa China iko tayari kufanya mazungumzo na Marekani ili kumaliza mvutano unaoendelea wa kibiashara, na kuwa China haitaki “ kuendeleza vita hivyo vya kibiashara.”

Mambo haya yaliyojitokeza yalisaidia kidogo sana kuimarisha masoko ya hisa nchini Japan, China na Hong Kong, ambayo hisa zao zilishuka Jumatatu.

XS
SM
MD
LG