Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 04, 2024 Local time: 11:30

Tanzania: Watetezi wa haki za binadamu wataka serikali ibuni sheria maalum ya ukatili dhidi ya wanawake


Wanawake wa Tanzania wakishiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Tanzania, March 8th, 2024
Wanawake wa Tanzania wakishiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Tanzania, March 8th, 2024

Watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania wameitaka serikali ya nchi hiyo kubuni sheria maalum kwa ajili ya kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na wasichana kutokana na kuwepo kwa ongezeko la kubwa la ukatili katika kipindi cha hivi karibuni hali inayoendelea kutia wasiwasi.

Huku watetezi hao wakisema sheria iliyopo bado ina mapungufu yanayoendelea kutoa nafasi ya wanawake kuendelea kufanyiwa ukatili.

Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ni miongoni mwa changamoto ambayo inaendelea kushuhudiwa sehemu mbali mbali nchini Tanzania, ukatili huo ukihusisha wa kimwili, kijinsia, kisaikolojia, na hata unyanyasaji wa wanandoa ambapo unaonekana kuongezeka.

Pili Shabani ni mkazi wa Kijichi Dar es Salaam ambaye aliishi na mume wake kwenye ndoa kwa miaka mitano na kulazimika kuivunja ndoa yake baada ya vitendo vya ukatili dhidi yake kukithiri ikiwemo kupigwa, unyanyasaji na vitendo vingine hapa anaeleza hali aliyopitia kwenye ndoa hiyo.

"Baada ya kama mwaka na nusu ndani ya ndoa mambo yalibadilika. mume wangu alikuwa ni mtu mkali sana, linapotokea tatizo kidogo alikuwa ni mtu ambaye atakukoromea sana, muda mwingine unakuta labda nimekosea katika kupika ananipiga ikafika mahali kwa kweli nikawa nimechoka vipigo, yaani ilikuwa inafika wakati kwamba... yaani nashindwa hata nielezee vipi ila ndoa ilinishinda kwahiyo nikaomba talaka nikarudi nyumbani kwetu," amesema Pili.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) inaonyesha katika kipindi cha miaka mitano (2018-2022) nchini Tanzania wanawake 2,438 walipoteza maisha yao kutokana na ukatili ikiwa ni sawa na wanawake 492 kwa mwaka na wanawake 43 kwa mwezi huku kwa mwaka 2023 ukionyesha ongezeko la wanawake 53 wanaofariki kila mwezi hali inayoleta wasiwasi.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu

Getrude Biabene ni Afisa mwandamizi wa masuala ya jinsia, wanawake, na watoto katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) anaeleza sababu ambayo imepelekea kuwepo kwa ongezeko la vitendo vya mauaji ni kutokana na watu kupitia vitendo vya ukatili na kutotoa taarifa mapema pamoja na mifumo ya haki haitoi msaada wa haraka kwa wanaopitia vitendo vya ukatili.

Biabene anasema: "Sababu ni watu kupitia vitendo vya ukatili na kutokutoa taarifa mapema kwahiyo inawapa nguvu wale wanaofanya vitendo hivyo kuhisi kwamba wapo salama na kuendelea kufanya zaidi kwahiyo hicho nacho kimekuwa changamoto, lakini kitu kingine kinachochangia mauaji ni mifumo yetu ya haki kutotoa msaada wa haraka kwa waathirika wa ukatili."

Mifumo ya Haki inakabiliwa na Changamoto

Biabene anaongezea kuwa mifumo ya haki iliyopo nchini inashindwa kutoa msaada wa haraka kwa wanawake wanaopitia vitendo vya ukatili kutokana na kesi kutumia muda mrefu kusikilizwa pamoja na watuhumiwa kupewa ruhusa ya kutolewa dhamana pale wanapofikishwa katika vyombo vya dola suala ambalo linaongeza zaidi madhara ya ukatili.

Fundikira Wazambi ambaye ni mkuu wa kitengo cha utafiti kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu amesema mfumo wa sheria kutokutoa msaada wa haraka umepelekea wananchi kuviona vitendo vya ukatili kama vitendo vya kawaida suala ambalo linaendelea kuongeza madhara zaidi kwa wanawake.

Wazambi ameeleza kuwa: "Suala zima la ukatili limeanza kuonekana ni jambo la kwaida na hivyo inachangia kuendelea kutokea kwa vitendo vya kikatili na hatimaye kupelekea kutokea kwa mauaji, wengine wakiachwa wakiwa na ulemavu wa kudumu na majeraha mbalimbali katika mwili lakini pia vilevile tuna mapungufu katika sheria moja wapo ya vitu ambavyo tumekuwa tukipigia kelele ni kuwa na sheria maalumu ya masuala ya ukatili."

Kukosekana kwa Takwimu

Hata hivyo changamoto nyingine inayoelezwa na Kituo cha Sheria na Haki za binadamu ni kukosekana kwa takwimu za jumla kutoka wizarani zinazo onyesha picha halisi ya kila mkoa ili kuweza kufahamu sehemu ambazo mauaji ya wanawake na ukatili umekithiri ili kuyapa kipaumbele katika kuyashughulikia.

Ujumbe wa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria

Suala ambalo Mkurugenzi wa Kituo cha sheria na haki za binadamu Anna Henga amesema kukoseka kwa takwimu za kila eneo inaleta ugumu katika namna ya kupambana na ukatili kutokana na kutofahamu maeneo gani yaliyoathirika zaidi pia inaleta ugumu katika ugawaji wa bajeti ya kushughulikia ukatili wa kijinsia.

Henga amesema: "Kukosekana kwa takwimu inapelekea kushindwa kupanga bajeti mahususi kwa ajili ya kushughulikia tatizo unashindwa kulishughulikia tatizo inavyopaswa kama hujajua takwimu zake kwasababu unakuwa haujui tatizo kwa ukubwa wake na kwa uhalisia lakini serikali ikitoa takwimu yenyewe itatoa kwa kijiji kwa kijiji au kata kwa kata sasa ikitoa kata kwa kata maana yake hata serikali yenyewe itaweza kuweka bajeti mahususi kupambana na hilo tatizo.

Katika kuhakikisha serikali inapambana ipasavyo na mauaji ya wanawake pamoja na ukatili, watetezi wa haki za binadamu wanashauri kuundwa kwa sheria maalumu kwaajili ya kupambana na ukatili wa kijinsia itakayoelezea kwa upana masuala mazima ya ukatili kutokana na sheria iliyopo kuyaacha baadhi ya mambo ikiwemo mauaji ya wanawake kama anavyoeleza Biabene.

Biabene alieleza kuwa: "Sheria ya ukatili wa kijinsia ni kitu ambacho kila siku tunasema tuwe na sheria maalum ya ukatili wa kijinsia itakayoweza kueleza kwa mapana na marefu masuala yote ya ukatili ambayo yapo yameelezwa kwenye sheria ya kanuni ya adhabu lakini yameelezwa kwa ufupi sana na kuna masuala mengi yameachwa ikiwemo haya masuala ya mauaji ya wenza yakae kabisa kwenye maalumu ya ukatili wa kijinsia au sheria ya ukatili wa majumbani."

Henga amemalizia kwa kuitaka jamii kujenga mazoea ya kuripoti matukio ya ukatili mapema pale tu yanapojitokeza ili kusaidia kuzuia madhara zaidi na kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi pale wanapohitajika kutoa ushahidi ili kuhakikisha kila mtu anapata haki yake na inakuwa funzo kwa wengine.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Amri Ramadhani, Dar es Salaam

Forum

XS
SM
MD
LG