Huko Afrika Mashariki sherehe mbali mbali zimefanyika ambako viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wanaharakati wamedai nyongeza za mishahara na kazi za uhakika huku viongozi wakiahidi kuongeza nafasi za ajira.
Nchini Kenya sherehe rasmi zilifanyika katika uwanja wa Uhuru Gardens mjini Nairobi ambako Rais William Ruto ametowa wito kwa viongozi wa nchi watekeleza mpango wa maendeleo uliotangazwa na serikali yake kwa ajili ya wananchi.
"Tuko na mpango wa Housing, tuko na mpango wa Universal Health Coverage, tuko na kilimo, na mimi niliwaeleza kwamba bila ya kudanganyana kufanya maandamano kwa ajili ya njaa, njaa haiwezi kupotea. mpaka twende shambani, tulime chakula, chakula kipatikane kwa wingi ndio tutaweza kupunguza gharama ya unga na chakula."
Nao wafanyakazi wa Tanzania wameeleza changamoto mbalimbali ambazo wamekuwa wakizipitia makazini na kubwa kati ya mambo wanaolalamika ni kuanzishwa kwa mpango wa kitita kipya cha bima ya afya kilichopelekea baadhi ya huduma kuondolewa katika mfuko huo pamoja na kuwepo na mpango mpya katika mifuko ya hifadhi ya jamii ambacho kinaelezwa kubana maslahi ya wastaafu.
Wafanyakazi hao wa Tanzania pia wamesema tangu utaratibu mpya wa kuhesabu mafao kuanza, umekuwa changamoto na kuelekeza kwamba wastaafu hulipwa asilimia 33 ya kiinua mgongo baada ya kustaafu, kutoka kiwango cha awali ambacho mstaafu alikuwa akilipwa asilimia 50 kwa awamu moja.
Suala ambalo linawafanya wastaafu wengi kulazimika kuishi maisha duni na kukata tama baada ya kustaafu kutokana na kupokea malipo hafifu ya kiinua mgongo.
Aidha katika kuadhimisha siku hiyo ya wafanyakazi, Tanzania imetoa ajira kwa wafanyakazi elfu 12 katika mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ulioko Rufiji mkoni Pwani.
Kupitia Mtandao wa X serikali ya Tanzania imesema asilimia 95 ya ajira hizo zimetolewa kwa wazawa na asilimia tano za wageni.
Katika nchi nyingine za Afrika Mashariki na kati wafanyakazi wamelalamikia mishahara midogo, ughali wa maisha na mazingira magumu ya kufanya kazi, wakiwataka viongozi wao kuongeza mishahara ili kuweza kukabiliana na maisha magumu yanayowakabili.
Forum