Mvua kubwa imenyesha Afrika Mashariki na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi ambayo yameharibu mazao, kusomba nyumba na kuwakosesha makazi maelfu ya watu.
Watu 210 walifariki nchini Kenya kutokana na “hali mbaya ya hewa,” wizara ya mambo ya ndani imesema katika taarifa, huku watu 22 wakifariki katika saa 24 zilizopita.
Zaidi ya watu 165,000 walikoseshwa makazi yao, taarifa hiyo imeongeza, huku wengine 90 hawajulikani walipo, na kuzua hofu kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka zaidi.
Kenya na nchi jirani ya Tanzania ambako watu 155 walifariki katika mafuriko, sasa zinajiandaa kukabiliana na kimbunga Hidaya, kinachosababisha mvua kubwa, upepo na mawimbi kwenye fukwe zao.
Mamlaka ya Tanzania imeonya Ijumaa kwamba Hidaya “kimejiimarisha kufikia kiwango cha kimbunga kikali,” saa tatu asubuhi kilipokuwa umbali wa kilomita 400 kutoka kusini mashariki mwa mji wa Mtwara.
Forum