Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 16:51

Tanzania: Dkt Slaa na wenzake waachiwa na polisi kwa dhamana


DR Wilbroad Slaa (Kwa hisani ya Akaunti ya Dr Slaa ya Facebook)
DR Wilbroad Slaa (Kwa hisani ya Akaunti ya Dr Slaa ya Facebook)

Mwanadiplomasia Wilbroad Slaa amewataka Watanzania kusimama imara katika kutetea na kulinda rasilimali za taifa ambazo zimekuwa zikinufaisha mataifa mengine huku wao wakiendelea kukabiliana na umasikini bila ya kupata manufaa kupitia rasilimali hizo.

Dkt Slaa ameyasema hayo muda mfupi baada ya kuachiwa kwa dhamana na jeshi la polisi lililokuwa likimshikilia kwa takribani siku tano.

Dkt Slaa anatuhumiwa na jeshi la polisi kwa uchochezi pamoja na makosa ya uhaini kufuatia kupinga uwekezaji wa bandari kati ya serikali ya Tanzania na Dubai, hivyo amewataka Watanzania kumuunga mkono kuendelea kulinda rasilimali za nchi kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadaye.

‘‘Kazi ya kupigania rasilimali za nchi ni ya Watanzania wote kwa mujibu wa ibara ya 27 moja na mbili kwa hiyo tusimame kidete kwa sababu rasilimali za nchi zinatumika tangu uhuru na mifano hai ni madini yametumika tumeachiwa mashimo na milima ya mchanga lakini madini yote yameisha,’’ amesema Dkt Slaa.

Licha ya kuachiliwa kwake Dkt Slaa amesema bado hafahamu kosa lililomfanya kukaa mahabusu kwa siku hizo kwa sababu kosa alilotuhumiwa halina dhamana kwa sheria za Tanzania.

‘‘Mimi mpaka sasa hivi sijaelezwa chochote nilikamatwa kwa makosa gani lakini makosa ya uhaini kwa mujibu wa sheria zetu hayana dhamana lakini nimepewa dhamana kwa hiyo hata mimi mwenyewe sijui tafsiri labda mtakapo ongea na wakili wangu yeye labda atawaambia ni kitu gani kimetokea kwa sababu hata mimi nimechanganyikiwa.’’ ameongezea Dkt Slaa

Kwa upande wa wakili Dickson Matata ameiambia Sauti ya Amerika kuwa mteja wake amepewa dhamana leo na kupewa masharti ya kutotoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam na kuendelea kuripoti kila atakapo hitajika.

‘‘Moja ya masharti ni kwamba watakuwa wanapangiwa tarehe za kwenda kuripoti lakini pia haturuhusiwi kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam mpaka kwa ruhusa ya RCO. ’’ amesema Matata

Kwa upande wa watuhumiwa wengine waliokamatwa pamoja na Dkt Slaa akiwemo wakili Boniface Mwabukusi na mwanachama wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mpaluka Nyagali waliokuwa wakishikiliwa na jeshi la polisi mkoani Mbeya wameachiwa kwa dhamana huku na wao wakipewa masharti ya kutotoka nje ya mkoa huo.

Hata hivyo Dkt Slaa amemalizia kwa kuwataka viongozi kuheshimu katiba ya nchi kwa vile kila mwananchi ana uhuru na haki ya kutoa maoni kwenye rasilimali zinazohusu taifa.

Amri Ramadhani Dar es Salaam

Forum

XS
SM
MD
LG