Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 22, 2024 Local time: 09:06

Serikali ya Tanzania yaombwa iwajumuishe wadau katika kuandaa bajeti


Bunge la Tanzania huko Dodoma Machi 30, 2021. Picha na AFP.
Bunge la Tanzania huko Dodoma Machi 30, 2021. Picha na AFP.

Bajeti ya serikali ya mwaka 2024/2025 iliyosomwa bungeni Alhamisi mjini Dodoma, serikali imeomba kuidhinishwa kwa jumla ya matumizi ya shilingi trillioni 49.35 ikiwa na ongezeko la asilimia 11 ikilinganishwa na bajeti ya 2023/2024.

Wakizungumza na Sauti ya Amerika baadhi ya wachumi wameishauri serikali kujenga utaratibu utakaowajumuisha wadau pamoja na wananchi katika uandaaji wa bajeti ili waweze kutoa maoni yao na kubaini vyanzo vipya vya mapato vitakavyowanufaisha

Dkt Ntui Ponsian ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Mtakatifu Agostino ameiambia Sauti ya Amerika kuwa utaratibu ambao umezoeleka nchini Tanzania unapaswa ufanyiwe mabadiliko kidogo, ili kuwepo na utaratibu ambao ni jumuishi zaidi.”

“Hii bajeti, kabla hata waziri hajaisoma ingepaswa angalau iweze kufika kwa wadau kwa sababu bajeti siyo siri kwa sababu haya mambo wananchi walipaswa watoe maoni na wangeweza kushauri vyanzo vingine vipya,” ameongezea Dkt Ponsian.

Wachumi wamesema kuwa licha ya serikali kuwa na kawaida ya kutengeneza bajeti ambazo ni nzuri na zinazotoa matumaini kwa wananchi, utekelezaji wa makadirio hayo umekuwa ukiwakatisha tamaa wananchi kutokana na bajeti hizo kutokutekelezwa kwa asilimia mia moja.

Wanawakewakipata mafunzo ya ushonaji Tanzania.
Wanawakewakipata mafunzo ya ushonaji Tanzania.

Dkt Visent Stanslaus mchumi na mhadhiri kutoka chuo kikuu huria cha Tanzania amesema bajeti za nyuma zimekuwa hazitekelezwi kikamilifu kutokana na malengo kutotimia hivyo wananchi wanatamani kuona matunda na matokeo ya bajeti zinazosomwa katika sekta mbalimbali.

“Yale mambo ambayo yanakuwa yamelengwa wakati mwingine hayatimizwi kwa asilimia mia moja kwa sababu ya fedha kutopelekwa kama ilivyokuwa imepangwa. Tulitarajia tuone utekelezaji wa bajeti iliyopita tulitaka tuone matokeo, mfano kwenye wizara ya kilimo matokeo yanaonekana,” alisema.

Hata hivyo, Dkt. Lutengano Mwinuka, Mhadhiri Mwandamizi wa idara ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Dodoma amesema Serikali inapaswa kubuni miradi ya ubia (PPP) na kuvutia sekta binafsi ili kusaidia majukumu ya kiserikali.

Mwinuka alisema: “Sasa hivi pamekuwa na mwitikio mzuri wa miradi ya ubia, na jinsi gani serikali zetu zinabuni miradi mizuri na mikubwa ambayo itavutia sekta binafsi na iweke mitaji, ikaweka ubunifu, ikaweka teknolojia lakini na uendeshaji wa miradi hiyo na itachangia kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.”

Wachumi wameisihi serikali kutengeneza bajeti ambazo zitatoa kipaumbele katika maeneo ambayo yanaweza kusaidia kuongeza pato la taifa kwa asilimia kubwa ili kupunguza utegemezi wa mikopo kutoka katika mataifa ya nje.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG