Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 12:35

Tanzania yaombwa kubuni mikakati ya uzalishaji bidhaa muhimu ndani ya nchi


Mfanyabiashara akiuza bidhaa mtaani katika jiji la Dar es Salaam. Picha na Ericky BONIPHACE / AFP.
Mfanyabiashara akiuza bidhaa mtaani katika jiji la Dar es Salaam. Picha na Ericky BONIPHACE / AFP.

Baadhi ya makampuni ya usafirishaji nchini Tanzania yametangaza ongezeko la gharama za usafirishaji wa mizigo kutoka China na Dubai hadi Dar es Salaam. Hali inayoleta wasiwasi wa kuongezeka kwa gharama za maisha kwa wananchi wa kipato cha chini.

Kufuatia hatua hiyo, baadhi ya Wachumi nchini humo wameitaka serikali kubuni sera ya kuchochea uzalishaji wa bidhaa muhimu ndani ya nchi ili kupunguza uagizaji wa nje, na kusaidia kuepusha ongezeko la bei kwa bidhaa pindi inapotokea changamoto katika mnyororo wa usambazaji.

Akizungumza na sauti ya Amerika, Joshua Lukonge, mchambuzi wa masuala ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema “Katika hii mitikisiko serikali inatakiwa ijihami kwa kuweka mipango ya kuhakikisha vile ambavyo tunaweza kuvizalisha hapa ndani viwekewe sera ya kuchochea uzalishaji.”

“Kwa sera tu ya serikali wanaweza wakafanya bidhaa fulani ambayo ilikuwa haizalishwi izalishwe sana kwahiyo ni vyema serikali kuhakikisha wanahamasisha uzalishaji wa bidhaa ambazo zikiguswa na huu mtikisiko wa mnyororo wa usambazaji tunakuwa na hali mbaya sana,” Amesema Lukonge.

Soko la Darajani lililoko Mji Mkongwe, Zanzibar
Soko la Darajani lililoko Mji Mkongwe, Zanzibar

Kwa mujibu wa Meneja Masoko wa kampuni ya Mo Cargo, Isihaka Masubi, kupanda kwa bei kunatokana na kukosekana kwa usalama katika safari za meli kutoka Ulaya kuja Afrika, hali inayosababishwa na mashambulizi yanayofanywa katika bahari ya Sham, na hivyo kusababisha gharama za usafirishaji kuongezeka kutoka Dola 2,800 hadi Dola 9,000.

Masubi anasema kutokana na sababu hizo za kiusalama, kumekuwa na upungufu wa makontena nchini China, uliosababishwa na baadhi ya meli kutafuta njia nyingine za kupita. Hali hii inapelekea meli kutumia siku nyingi zaidi majini, hivyo kusababisha kuchelewa kuwasili kwa mizigo.

“Sababu kuu inayosababisha kupanda kwa bei ya usafirishaji wa mizigo ni kukosekana kwa makontena nchini China, sababu ya kukosekana kwake inatokana na vita na wale mashambulizi yanayoanywa kwenye bahari ya Sham inapelekea meli nyingi kuzunguka na kuchelewesha kurudisha makontena nchini china,” alisema Masubi.

Meli ya mizigo ikiwa katika bandari ya Zhoushan huko mashariki mwa jimbo la Zhejiang huko China .
Meli ya mizigo ikiwa katika bandari ya Zhoushan huko mashariki mwa jimbo la Zhejiang huko China .

Hata hivyo, kwa upande wa wafanyabiashara, kupitia Mwenyekiti wao katika soko la kimataifa la Kariakoo jijini Dar es Salaam, Martine Mbwana, wametoa wito kwa serikali kuangalia upya makadirio ya kodi katika kipindi hiki cha dharura ya kupanda kwa gharama za usafirishaji. Wamesema hatua hii ni muhimu ili kuepusha mfumuko wa bei za bidhaa.

Alisema “Tunatoa wito kwa serikali iangalie kwenye uthaminishaji wa mizigo, unapothaminisha mizigo bandarini mzigo unapoingia kuna gharama za mzigo na usafirishaji sasa gharama za usafirishaji zikiwa kubwa thamani ya mzigo pia inakuwa kubwa kwahiyo kodi zinatoka kubwa zaidi sasa waangalie namna ya kuweza kukadiiria kwenye mizigo kwa dharula,”

Hata hivyo Lukonge alisema kuwa kupanda kwa gharama za usafirishaji kutawaathiri wananchi kwa sababu bei za bidhaa zitaongezeka, na serikali itapoteza mapato ya kodi kutokana na wafanyabiashara kupunguza uagizaji wa mizigo.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika, Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG