Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 19:13

Ruto aahidi kuchangia masuala muhimu ya Afrika Mashariki, kuendeleza amani


Rais mteule wa Kenya William Ruto akiongea baada ya Mahakama ya Juu kuhalalisha ushindi wake katika uchaguzi wa urais 2022, akiwa Nairobi, Sept. 5, 2022.
Rais mteule wa Kenya William Ruto akiongea baada ya Mahakama ya Juu kuhalalisha ushindi wake katika uchaguzi wa urais 2022, akiwa Nairobi, Sept. 5, 2022.

Rais mteule wa Kenya William Ruto ametoa mwanga wa agenda ya sera yake ya mambo ya nje katika mahojiano aliyofanya na kituo cha televisheni cha  Marekani CNN Jumatano, akiahidi kuongeza mchango wa nchi hiyo katika juhudi za usalama wa kikanda.

Dkt Ruto, ambaye anatarajiwa kuapishwa Septemba 13, hakudokeza chochote kuhusu mabadiliko yoyote makubwa ya sera ya mambo ya nje kutoka ile ya mtangulizi wake Uhuru Kenyatta. Sherehe za kuapishwa kwake zitafanyika katika uwanja wa michezo wa Kasarani mjini Nairobi.

Dkt Ruto anachukua kijiti cha kuiongoza Kenya huku kukiwa na changamoto na fursa nyingi nchi humo, kikanda na eneo kubwa la Pembe ya Afrika.

Anaweza kutumia mafanikio ya kidiplomasia ya mtangulizi wake – Uhuru Kenyatta – yaliyofanyika katika muingiliano wa kikanda na kuiweka Kenya katikati ya amani ya kikanda na miradi ya kiusalama, au kuamua kufuata njia yake mwenyewe kwa kutumia fagio jipya la kisiasa na kiuchumi.

Rais anayeondoka madarakani Uhuru Kenyatta.
Rais anayeondoka madarakani Uhuru Kenyatta.

Katika ilani yake ya kisiasa, Dkt Ruto anasema chama chake cha Kenya Kwanza Alliance kina nia ya dhati kwa muingiliano wa kikanda ambao utaifanya Kenya kituo muhimu katika kanda hiyo.

“Serikali ya Kenya Kwanza itahakikisha kuwa nchi inaheshiwa na kuthaminiwa kote ulimwenguni. Itahamasisha mahusiano ya kirafiki na jirani zake, itachukua nafasi ya mbele katika masuala ya kikanda na barani Afrika, itashirikiana na washirika wake wa kimataifa, na kuendelea kuimarisha ahadi zetu kwa jumuiya ya kimataifa,” ilani hiyo inaeleza katika kifungu cha sera ya mambo ya nje.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo bado ni changamoto. Wakati Uhuru alikuwa amefuata sera ya kupunguza vita upande wa mashariki mwa DRC, Dkt Ruto anaanza kutoka hatua isiyotabirika katika mahusiano yake na nchi ya pili kubwa barani Afrika na kiongozi wake, Felix Tshisekedi.

Rais Félix Tshisekedi wa DRC akiwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, mjini Nairobi, Februari 6, 2019. (Twitter/Uhuru Kenyatta)
Rais Félix Tshisekedi wa DRC akiwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, mjini Nairobi, Februari 6, 2019. (Twitter/Uhuru Kenyatta)

Rais Kenyatta alikuwa kati ya viongozi wachache wa Afrika waliohudhuria kuapishwa kwa Rais Tshisekedi mjini Kinshasa wakati viongozi wengine wa Afrika na Umoja wa Afrika (AU), walikuwa na shaka kuhusu ushindi wake dhidi ya Martin Fayulu.

Hivi karibuni Rais Kenyatta alikuwa mwenyeji wa wakuu wa nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadili kuzorota kwa usalama huko mashariki mwa DRC na kufanya bidii kuundwa kwa Kikosi cha Dharura cha Afrika Mashariki, na upelekaji wa wanajeshi nchini DRC.

Pia aliweka nia ya dhati ya kutuliza hali ilivyo huko mashariki mwa DRC kwa kupeleka wanajeshi 200 wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kukabiliana na wanamgambo wanaosababisha vurugu kwa raia na kutishia uwepo wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Chanzo cha habari hii ni gazeti la “The East African” linalochapishwa Kenya.

XS
SM
MD
LG