Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 00:11

Mahakama ya juu Kenya inatoa uamuzi Jumatatu kesi ya matokeo ya urais


Jaji wa mahakama ya juu Kenya, Martha Koome
Jaji wa mahakama ya juu Kenya, Martha Koome

Mahakama ya Upeo nchini Kenya inatarajiwa kutoa uamuzi siku ya Jumatatu kuamua kuhusu masuala yaliyoibuliwa na walalamishi kuhusu uadilifu wa uchaguzi wa Agosti 9 na uhalali wa kumtangaza Naibu Rais William Ruto kuwa Rais mteule.

Iwapo wengi wa majaji watatupilia mbali malalamiko yalioibuliwa na Mgombea wa Urais kupitia Muungano wa Azimio One Kenya, Raila Odinga na kuunga mkono matokeo yaliyotangazwa na baraza la uchaguzi, Rais Mteule William Ruto basi ataapishwa Septemba 13 kuchukua nafasi ya Uhuru Kenyatta na kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya .

Lakini iwapo watabatilisha ushindi wa William Ruto mamlaka zitakuwa na siku 60 kufanya uchaguzi mpya iwapo mahakama itatoa uamuzi unaomuunga mkono Odinga, ambaye tayari amepinga matokeo ya urais mara tatu katika maisha yake ya kisiasa ya muda mrefu na kuyataja matokeo ya kura ya hivi punde kuwa "upotovu".

Na Iwapo mahakama itakubali maombi ya Raila Odinga ya kutaka mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati afunguliwe mashtaka na kuzuiwa kuendesha uchaguzi wa marudio, itachukua muda mrefu kufanya uchaguzi mpya.

Tayari baadhi ya wakenya wameelezea kukosa imani na Tume ya IEBC kufuatia migawanyiko ya ndani, ambayo imeshuhudia kundi moja la makamishna wakikataa matokeo yaliyotangazwa na Mwenyekiti Wafula Chebukati .

Wiki iliyopita kundi la Muungano wa Azimio One Kenya pamoja na wanasheria wa Odinga waliwasilisha kesi wakidai kuwa mfumo wa uchaguzi Nchini kenya ulikubwa na dosari nyingi pamoja ya Uingiliwaji wa Teknolojia za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC n na kubadilisha picha halisi za fomu za matokeo ya vituo vya kupigia kura na kuweka za uwongo, hivyo basi kuongeza mgao wa Ruto katika kura ya Agosti 9.

Aidha ombi la Odinga pia lilidai kuwa matokeo ya Urais ni batili kwa sababu yalitangazwa na mwenyekiti badala ya tume nzima huku Odinga akitaka mwenyekiti wa IEBC abadilishwe.

Kwa upande wa Mawakili wa IEBC na William Ruto walimshutumu Odinga kwa kughushi kumbukumbu za kompyuta ili kuleta mgogoro wa kikatiba na kulazimisha makubaliano ya kugawana mamlaka.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi amesema uchaguzi ulikuwa "huru, haki na wa kuaminika" katika majibu yake ya mahakama huku Makamishna wanne wapinzani wakiwasilisha majibu ya kuibua wasiwasi kuhusu mchakato wa kujumlisha kura na mienendo ya mwenyekiti.

Baada ya kusoma maombi yaliowasilishwa, Mahakama ya Upeo ikiongozwa na Jaji Mkuu na Rais wa Mahakama ya Juu Martha Koome ilipunguza madai na kadhia nyingi katika kesi nane za kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 9 hadi masuala tisa ambayo matokeo yake yataamua iwapo Ushindi wa Ruto utaidhinishwa.

Baada ya kukamilika kwa mvutano wa mawakili, macho yote sasa yanawaangazia majaji hao kutoa uamuzi ambao utaamua mustakabali wa taifa la Kenya.

XS
SM
MD
LG