Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 20:22

Ahadi za Dr. William Ruto zilizompa ushindi dhidi ya Raila Odinga


Rais mteule wa Kenya Dr. William Ruto
Rais mteule wa Kenya Dr. William Ruto

Rais mteule wa Kenya William Ruto aliahidi mambo mengi wakati wa kampeni, alipokuwa akitafuta kura kuelekea ikulu.

Ilani ya Ruto inazingatia ujenzi wa uchumi thabithi, kuimarisha elimu, afya, teknolojia, ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na sekta ya kilimo.

Ruto amekuwa akisisitiza kwamba changamoto zinazoikumba Kenya kwa sasa zinastahili kushughulikiwa kwa haraka sana na kwamba lengo lake kubwa ni kuimarisha ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo, ambao unaendelea kupambana na athari za janga la virusi vya Corona.

Ameelezea kwamba atatumia mbinu tofauti za kuimarisha ukuaji wa uchumi huo ilivyo tofauti na jinsi mambo yanavyofanyika kila mara, na kumhusisha kila Mkenya katika ujenzi wa taifa hilo.

Uchumi unaokua kwa kuzingatia zaidi watu wa kipato cha chini.

Kulingana na Ruto, mfumo wa uchumi kutoka kwa watu wenye kipato cha juu ukishuka hadi kwa watu wenye kipato cha chini haufai, na kwamba mfumo bora ni kuangazia zaidi watu wenye kipato cha chini ambao idadi yao ni kubwa sana nchini Kenya ikilinganishwa na wenye kipato cha juu.

“Kwa kuhakikisha kwamba kila mtu anashirikishwa katika maswala yanayohusu wananchi na kutambua sehemu muhimu katika ujenzi wa taifa na jamii, mfumo huo unahakikisha kwamba kazi inayotekelezwa na serikali inatosheleza mahitaji ya watu wake,” amesema Ruto.

Maendeleo kutoka mashinani

Ruto amesema kwamba mfumo wa ukuaji wa uchumi unaozingatia sana watu wenye kipato cha chini, ambao umejulikana sana Kenya kwa lugha ya kiingereza ‘Bottom up’, utatekelezwa kutoka kwa serikali za kaunti 47 za Kenya.

Kaunti zote zitazingatia sekta muhimu za kilimo, upatikanaji wa chakula, ukuaji wa biashara ndogo ndogo, ujenzi wa nyumba, afya, teknolojia na ubunifu.

Utawala wa Ruto utazingatia yafuatayo

Amesisitiza kuhusu kulinda katiba ya Kenya, kubuni mazingira ya ajira kwa wakenya,kufufua uchumi, kuboresha utendakazi wa idara ya mahakama, kuimarisha kiwango cha elimu, kuboresha mfumo wa afya, kuwateua majaji wote walioachwa nje na rais Uhuru Kenyatta ndani ya siku saba iwapo atateuliwa kuwa rais katika uchaguzi wa Agosti 9.

Ruto pia ameahidi kuanzisha Mfuko Maalum wa Fedha kufadhili biashara ndogondogo zinazoongozwa na wanawake na vijana, pamoja na kuunda nafasi za kazi katika sekta ya kilimo.

Nafasi za vijana na wanawake serikalini

Dr. William Ruto ameahidi kuwa na angalau asilimia 50% ya wanawake katika baraza lake la mawaziri huku akiahidi kuwa nyadhifa za uteuzi katika sekta ya umma zitazingatia kanuni ya theluthi mbili ya jinsia.

"Vijana wetu na wanawake, ndio nguzo ya mpango wetu. Tumeweka ahadi na vijana wa nchi hii kwamba tutaunda wizara maalum kwa ajili ya vijana. Tutakuwa na mshauri mkuu katika ofisi ya rais kuhakikisha kwamba mipango yote ya serikali inawashirikisha vijana. Kama muungano wa Kenya kwanza, tumekubaliana kwamba asilimia 50 ya baraza la mawaziri watakuwa wanawake. Tumekubaliana kwamba vijana na wanawake watafaidika sana na mfuko maalum wa kuinua biashara ndogo ndogo." Alisema Ruto alipokuwa akizindua ilani yake.

Ahadi kuu za William Ruto kwa Wakenya

  • Kutenga shilingi bilioni 259 kwa ajili ya kuimarisha kilimo na kuhakikisha kuna chakula cha kutosha.
  • Kujenga nyumba 250,000 za gharama nafuu kila mwaka kwa ushirikiano na sekta binafsi
  • Kila mkenya kuwa na bima ya afya
  • Shilingi bilioni 50 kila mwaka kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo ambao watapata mikopo kwa njia rahisi.
  • Kuweka mfumo maalum wa kifedha kwa ajili ya kuwapa makazi watu milioni moja wasiokuwa na ardhi.
  • Kuajiri wadaktari na wafanyakazi wa afya 20,000
  • Kuajiri walimu zaidi wanaohitajika ili kuziba pengo lililopo kwa sasa.
  • Kukamilisha ujenzi wa barabara zote ambazo zinajengwa kwa sasa
  • Kujenga kilomita 100,000 za mfumo wa internet yani ‘fibre optic.’
  • Kuwateua majaji wa mahakama ya juu, walioidhinishwa na tume ya kuwaajiri majaji JSC, ndani ya siku saba baada ya kuapishwa.

Bilioni 50 kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo

Katika upatikanaji wa fedha, Ruto aliahidi kutenga shilingi bilioni 50 kila mwaka kufadhili biashara ndogondogo na kuzipa fursa ya 100% ya kupata fedha nafuu kupitia vyama vya ushirika, akiba na mikopo na kuwepo kwa mtaji, fedha za hisa na mikopo ya muda mrefu kuwawezesha wafanyabiashara kuanzisha na kukuza biashara hizo.

Ruto amekuwa akiukosoa utawala wa rais wa sasa Uhuru Kenyatta kwa kile alichodai kutumia taasisi za kufuatilia makosa ya jinai, visivyo, amesema kuwa serikali yake itaanzisha mfuko huru wa kifedha kwa tume ya kupambana na rushwa EACC na idara ya polisi ili kukoma kupata maagizo na ufadhili kutoka kwa ofisi ya rais.

Uhuru wa mahakama

Na ili, kuimarisha uhuru wa mahakama, Ruto vile vile anaahidi kuiwezesha idara ya mahakama kujitegemea kuendesha shughuli zake bila kuitegemea ofisi ya rais.

Wakati akizindua ilani yake, Ruto alisema kuwa katika kipindi cha siku saba baada ya kuchaguliwa kuwa rais, atawateua majaji wote waliopendekezwa na tume ya huduma za mahakama kwa rais.

Kuajiri walimu 116,000

Kuhusu elimu, Ruto aliahidi kupunguza pengo la sasa la upungufu wa walimu 116,000 ndani ya miaka miwili ya fedha, kukagua mfumo wa sasa unaoegemea mitihani wa kuendelea na masomo, ambao anasema haujajumulisha mamilioni ya wanafunzi kulingana na mitihani ya kumaliza elimu ya msingi, kwa kutekeleza njia mbadala vigezo vya kuingia.

"Sekta yetu ya elimu inakumbana na changamoto chungu nzima hasa elimu ya juu. hakuna ufadhili wa kutosha."

Ruto amewania urais kwa mara ya kwanza kabisa baada ya kuhudumu mihula miwili kama naibu rais wa Kenya chini ya utawala wa rais Kenyatta.

Ruto ameweka historia.

Ruto amekuwa naibu rais wa kwanza katika historia ya Kenya kushinda uchaguzi wa urais. Ilani yake ya uchaguzi inazingaita vigezo tano; Kilimo, Uchumi wa Biashara ndogondogo na za Kati, Nyumba na Makazi, Huduma ya afya na mahimizo ya uchumi kidigitali na bunifu.

XS
SM
MD
LG