Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 00:38

Ukraine: Russia yawauliza wakazi wa mikoa inayoikalia kimabavu kama wanataka kuwa chini ya utawala wake


Watu wakisubiri kupiga kura ya maoni katika kituo cha muda cha kupiga kura huko Luhansk, Ukraine, Ijumaa, Sept. 23, 2022.
Watu wakisubiri kupiga kura ya maoni katika kituo cha muda cha kupiga kura huko Luhansk, Ukraine, Ijumaa, Sept. 23, 2022.

Zoezi la kura ya maoni iliyopangwa na Russia limeanza katika mikoa inayoikalia nchini Ukraine, ikiwauliza wakazi wa huko kama wanataka mikoa yao iwe ni sehemu ya Russia.

Upigaji kura ulianza Ijumaa huko Luhansk, Kherson na katika baadhi ya mikoa ya Zaporizhzhia na Donetsk inayodhibitiwa na Russia.

Upigaji kura huo, unachukuliwa kama njia ya Russia kutaka kuhalalisha uvamizi kwenye mikoa hiyo, zoezi ambalo limelaaniwa kwa wingi na nchi za Magharibi.

Watu wakiendelea kupiga kura katika maeneo ya mikoa ya Ukraine inayokaliwa kwa mabavu na Russia.
Watu wakiendelea kupiga kura katika maeneo ya mikoa ya Ukraine inayokaliwa kwa mabavu na Russia.

Jumuiya ya Usalama na Ushirikiano Ulaya, OSCE, imesema kura hiyo ya maoni si halali.

“Uchaguzi au kura ya maoni katika ardhi ya Ukraine unaweza kutangazwa na kufanywa na maafisa halali, kulingana na sheria za taifa na viwango vya kimataifa, Jumuiya ya OSCE ilisema katika taarifa yake. “Hivyo kura ya maoni iliyopangwa’ itakuwa ni uvunjifu wa sheria.”

Upigaji kura wa Ijumaa unafuatia tangazo lililotolewa na Rais wa Russia Vladimir Putin kuwa anakusudia kuwaandikisha wanajeshi wa akiba 300,000 kwa ajili ya “operesheni maalum za kijeshi” huko Ukraine.

Rais Vladimir Putin
Rais Vladimir Putin

Putin alisema katika hotuba iliyotangazwa kupitia televisheni wiki hii kwamba kuandikishwa wanajeshi wa akiba, ni muhimu katika kulinda mipaka na utawala wa Russia, na hiyo inaonekana ni kufuatia mafanikio ya Ukraine katika kujibu mashambulizi ya Russia huko kaskazini mashariki mwa Ukraine.

Putin alisema nchi za Magharibi zinajaribu kudhoofisha na kuiangamiza Russia, na kuwa nchi yake itatumia “kila nyenzo iliyoko katika mikono yetu kuilinda Russia na watu wetu.”

Maandamano ya mitaani dhidi ya kuandikishwa wanajeshi yamezuka Moscow na miji mingine ya Russia, huku polisi wakiwakamata waandamanaji 1,300.

Wakati huo huo Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema katika ripoti yake ya kijasusi Ijumaa: “Katika siku tatu zilizopita, majeshi ya Ukraine yamedhibiti ngome muhimu ya kivita huko ukingo wa mashariki ya mto Oskil katika eneo la Kharkiv Oblast. Upande wa kusini, huko Donetsk Oblast, mapigano yanaendelea wakati majeshi ya Ukraine yakiushambulia mji wa Lyman, mashariki mwa Mto Siverskyy, ambao ulitekwa na Russia mwezi Mei. Hali ya uwanja wa vita bado ni tete, lakini Ukraine hivi sasa inashinikiza kukamata ardhi ambayo Russia inaiona ni muhimu kwa malengo yake ya kivita."

XS
SM
MD
LG