Alionya nchi za magharibi kwamba alikuwa hafanyi utani aliposema kuwa atakuwa tayari kutumia zana zote walizonazo kuilinda Russia.
Katika hatua kubwa kabisa ya kutaka kuongeza vita vya Ukraine tangu uvamizi wa Moscow Februari 24, Putin amefafanua kwa uwazi kabisa uwezekano wa vita vya nyuklia, alipoidhinisha mpango wa kuteka sehemu kubwa ya Ukraine yenye ukubwa wa Hungary, na kutoa wito kwa askari wa akiba 300,000.
“Ikiwa usalama wa mipaka yetu utatishiwa, bila shaka tutatumia njia zote zilizopo kuilinda Russia na wanainchi wetu, huu sio utani,” Putin amesema katika hotuba kwa taifa kwa njia ya televisheni.
Akitaja mfano wa kupanuka kwa muungano wa NATO kuelekea mipaka ya Russia, Putin amesema nchi za magharibi zinapanga kuiangamiza nchi yake, zikijihusisha na uhasama wa nyuklia, kwa madai ya kujadili uwezekano wa matumizi ya silaha za nyuklia dhidi ya Moscow, na kuzishtumu Marekani, Umoja wa Ulaya na Uingereza kwa kuihimiza Ukraine kuendesha operesheni za kijeshi ndani ya Russia.