Trump alianza safari ya kurejea Marekani mapema leo kwenye uwanja wa ndege wa kijeshi wa Bagram baada ya kuwa na wanajeshi wa Marekani kwa saa kadhaa pamoja na mkutano mfupi na Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, Trump amesema kuwa Marekani imekuwa kwenye mazungumzo na kundi la Taliban na anatumai kuwa linazingatia amani.
Trump kwa ghafla alisitisha mpango wa mkutano na Taliban mwezi Septemba kwenye eneo la kitalii la Camp David hapa Marekani baada ya bomu lililodaiwa kupigwa na kundi hilo kuuwa watu 12 mjini Kabul akiwemo mwanajeshi mmoja wa Marekani.
Haijabainika ni kwa muda gani tangu wakati huo, ambapo Marekani imekuwa ikishauriana na Taliban.
Msemaji wa ikulu ya Marekani Judd Deere amesema kuwa rais wa Afghanistan alifahamishwa kuhusu ziara za Trump muda mfupi tu kabla ya kuwasili Afghanistan.
Wakati akiwa Afghanistan, Trump alihutubia zaidi ya wanajeshi 15,000 wa Marekani akiwaambi kuwa alisafiri kwa zaidi ya kilomita 8,331 ili kushiriki nao kwenye siku kuu ya Thanksgiving akiwa na ujumbe kuwa Marekani inaendelea kuimarika.