Rais wa Marekani Donald Trump alifanya ziara ya kushtukiza kwenda Iraq kuwatembelea wanajeshi wa Marekani waliopo huko. Hii ni ziara yake ya kwanza kama rais kutembelea eneo hilo lenye mzozo.
Msemaji wa White House, Sarah Sanders alisema kwamba Rais Trump na mkewe Melania Trump walisafiri kwenda Iraq kuwashukuru wanajeshi wa Marekani kwa huduma zao, mafanikio yao na kujitoa kwao na pia kuwatakia kheri ya Christmas.
Ziara ya rais huko Iraq imekuja siku moja baada ya Trump kufanya mazungumzo kwa njia ya video kutoka White House na wanajeshi wa Marekani walioko sehemu mbali mbali. Baada ya mazunguzo hayo alikosolewa na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo viliripoti kwamba Trump alikuwa rais wa kwanza tangu mwaka 2002 kutotembelea wanajeshi wa Marekani wakati wa Christmass.
Wiki iliyopita Trump alifanya maamuzi yenye utata kutangaza mipango ya kuondoa wanajeshi wa Marekani kutoka Syria. Pia aliripotiwa kuiamurisha Pentagon kuondoa takribani nusu ya zaidi ya wanajeshi wa Marekani 14,000 walioko kwenye vituo nchini Afghanistan, kuanzia Januari 2019.
Washauri waandamizi wa Rais Trump na maafisa wa jeshi wanaonya hatua hiyo italitumbukiza zaidi eneo kwenye vurugu.