Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:47

Kenya : Rais Kenyatta kuunda jopo la uteuzi wa makamishna IEBC


Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anatarajiwa wiki hii kuunda jopo la uteuzi la makamishna wanne wa Tume ya Uchaguzi, IEBC, kujaza nafasi za makamishna wanne waliojiuzulu baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Tume ya uchaguzi (IEBC) hivi sasa ina makamishna watatu pekee. Ripoti ya BBI inapendekeza haja ya kuwa na makamishna wapya kwa tume hiyo kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kenya (IEBC) Wafula Chebukati (C), akiwa na makamu wake Connie Nkatha (kushoto) na Kamishna Paul Kurgat, Nairobi, Kenya, Oct. 25, 2017.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Kenya (IEBC) Wafula Chebukati (C), akiwa na makamu wake Connie Nkatha (kushoto) na Kamishna Paul Kurgat, Nairobi, Kenya, Oct. 25, 2017.

Makamishna waliojizulu katika tume hiyo ni Dkt Roselyn Akombe, Connie Nkatha Maina ambaye alikuwa Naibu Mwenyekiti, Dkt Paul Kibiwott Kurgat na Margaret Mwachanya kwa kile walichokidai kuwa ni kuingiliwa kwa tume hiyo na watu kutoka nje kwa kuishinikizia maamuzi. Hii ni kufuatia uchaguzi mkuu wa 2017 ambao ulibatilishwa na mahakama ya juu Kenya.

Tangu wakati huo tume ya IEBC imekuwa ikiendesha shughuli zake bila kuwapo kwa idadi inayohitajika kufanya maamuzi muhimu kwani ni makamishna watatu pekee waliopo; Wafula Chebukati, ambaye ni Mwenyekiti wa tume hiyo, Boya Molu na Profesa Abdi Yakub Guliye, wakati sheria inahitaji kuwepo makamishna saba.

Wafula Chebukati
Wafula Chebukati

Tangazo la Rais Kenyatta kupitia gazeti la serikali, wiki jana la kutangaza wazi nafasi nne za makamishna hao, linatoa nafasi kwake kubuni jopo la kujaza nafasi hizo katika kipindi cha wiki mbili.

Hadi Ifikapo Jumatano, Kenyatta, anatarajiwa kupokea majina saba yaliowasilishwa kwake na Spika wa Bunge la Taifa Justin Muturi ili kuanzisha mchakato wa kujaza nafasi hizo, takriban miezi 15 kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Hata hivyo, haifahamiki, ni kwa nini Kenyatta ametangaza uwazi wa nafasi hizo hivi sasa takriban miaka minne baada ya wanne hao kujiuzulu wakati sheria inamtaka kuzitangaza katika muda wa siku saba baada ya kupokea barua za kujiuzulu.

Lakini mchambuzi wa siasa za Kenya, Michael Agwanda, anaeleza kuwa huenda kuna ugumu wa kutekeleza majukumu yao katika kipindi kilichobakia kabla ya uchaguzi mkuu.

“Pamekuwa na shinikizo la kuondoa makamishna watatu waliopo na kuwa na tume mpya—ikiwa ni sehemu ya ripoti ya mapendekezo ya mabadiliko ya katiba ya Kenya, kupitia mchakato wa BBI, inayopendekeza kuteuliwa kwa makamishna wapya. Lakini Bw Agwanda anaeleza kuwa hili huenda likaleta utata.

Kwa upande wake Kevin Osido, mtaalam katika masuala ya uongozi nchini Kenya anaeleza kuwa mchakato mzima huenda ukawa na nia ya kufanya mabadiliko makubwa katika tume hiyo yanayojumuisha kuondolewa mwenyekiti wake Wafula Chebukati.

“Makamishna hawa wamekuwa wakilaumiwa kwa kuvuruga uchaguzi wa rais 2017 na utendaji kazi pamoja na mwenyekiti wake umetiliwa shaka, madai ambayo IEBC imeyakana. Lakini Osido anaeleza kuwa huenda serikali inahitaji maafisa watakaounga mkono juhudi zake za mabadiliko ya katiba,” ameongeza Chebukati.

Wakati huohuo Rais Kenyatta amemteua Consolata Nkatha Maina kuwa naibu balozi wa Kenya katika mjini Rome nchini Italia, Paul Kurgat Kibiwott ameteuliwa kusimamia ubalozi wa Kenya katika mjini Moscow, nchini Russia naye Margaret Mwachanya ameteuliwa kuiwakilisha Kenya nchini Pakistan kuwa naibu balozi wa Kenya.

Ripoti imetayarishwa na Kennedy Wandera.

XS
SM
MD
LG