Putin, ambaye yuko katika ziara ya siku mbili nchini China, aliutaja uhusiano huo kama chanzo cha utulivu duniani, na akasema ushirikiano wa nchi hizo mbili "hauelekezwi dhidi ya mtu yeyote," kulingana na shirika la habari la serikali la RIA Novosti.
Putin alitoa shukrani kwa China kwa kile alichokiita juhudi za nchi hiyo za kutatua mzozo wa Ukraine na kusema atamjulisha Xi kuhusu maendeleo ya hivi karibuni.
Russia iliivamia Ukraine mwezi Februari mwaka 2022, na kulaaniwa kimataifa, na kuwekewa vikwazo na mataifa ya Magharibi vilivyolenga kushinikiza Putin kuondoa vikosi vyake.
Shirika la habari la serikali ya China Xinhua lilimnukuu Putin akisema Jumatano kwamba Russia "haijawahi kukataa kujadili" utatuzi wa mzozo huo, na kwamba inatafuta "suluhisho la kina, endelevu na la haki la mgogoro huo kwa njia za amani."
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amependekeza mpango wa amani, na Uswisi inatazamiwa kuandaa mazungumzo ya amani mwezi ujao, lakini Russia haikualikwa kwenye mikutano hiyo. Ukraine inataka kuondolewa kabisa kwa vikosi vya Russia kutoka Ukraine, ikiwa ni pamoja na kutoka katika maeneo ambayo Russia ilidai kunyakua, katika hatua ambayo ilipingwa na jumuiya ya kimataifa.
Forum