Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 09:10

Nyama inayozalishwa kwenye maabara yakabiliwa na upinzani Marekani


Nyama iliyozalishwa katika maabara
Nyama iliyozalishwa katika maabara

Nyama inayozalishwa maabara kwa sasa bado haipatikani katika maduka au migahawa yoyote nchini Marekani. Ikiwa baadhi ya wabunge watafaulu kupiga vita uzalisha huo.

Mapema mwezi huu, majimbo ya Florida na Arizona zilipiga marufuku uuzaji wa nyama na samaki inayozalishwa kwa kutumia seli za wanyama. Huko Iowa, gavana alisaini muswada unaozuia shule kununua nyama inayozalishwa maabara. Wabunge wa serikali kuu pia wanatafuta kupitisha muswa wa kuzuia bidhaa hiyo.

Haijulikani jinsi juhudi hizi zitakavyokwenda mbali. Baadhi ya kampuni za nyama inayozalishwa zinasema zinafikiria kuchukua hatua za kisheria, na baadhi ya majimbo - kama Tennessee - yameweka kando marufuku zilizopendekezwa baada ya wabunge kusema zitawazuia watumiaji kufanya uchaguzi.

Hata hivyo, inaonekana kuwa ni mwisho wa matumaini makubwa kwa sekta ya nyama inayozalishwa baada ya jitihada zao mapema mwaka huu.

Marekani iliidhinisha uuzaji wa nyama inayozalishwa maabara kwa mara ya kwanza mwezi Juni 2023, ikiruhusu kampuni mbili za California, Good Meat na Upside Foods, kuuza kuku iliyozalishwa maabara. Migahawa miwili ya hadhi ya juu nchini Marekani iliongeza bidhaa hizo kwenye menyu zao kwa muda mfupi. Baadhi ya kampuni za nyama inayozalishwa zilianza kupanua uzalishaji. Bidhaa moja ya Good Meat ilianza kuuzwa katika duka moja la vyakula nchini Singapore.

Lakini uzalishaji huo hujaenda mbali, wanasiasa walianza kuweka vikwazo. Wabunge katika majimbo saba wanatafuta kupitisha miswada ya sheria zinazopiga marufuku nyama inayozalishwa, kulingana na Kim Tyrrell, mkurugenzi msaidizi wa Mkutano wa Kitaifa wa Mabunge ya Majimbo.

Katika Seneti ya Marekani, Maseneta wa Republican Jon Tester wa Montana na Mike Round wa South Dakota pia walipendekeza muswada mwezi Januari wa kupiga marufuku matumizi ya nyama inayozalishwa maabara katika programu za chakula za shule.

Pingamizi hizi sio Marekani pekee. Italia ilipiga marufuku uuzaji wa nyama inayozalishwa mwishoni mwa mwaka jana. Wabunge wa Ufaransa pia walitambulisha muswada wa kuipiga marufuku.

Shinikizo hilo linakuja ingawa nyama inayozalishwa maabara na samaki bado hazijafikia soko na pia kwa sababu ni ghali sana kuzalishwa. Bidhaa hizo huzalishwa kwenye matangi ya chuma kwa kutumia seli kutoka kwa mnyama aliye hai, yai lililotungwa au chombo cha kuhifadhi seli. Seli hulishwa mchanganyiko maalum wa maji, sukari, mafuta na vitamini. Mara baada ya kukua, huundwa kuwa vipande, na maumbo mengine.

Kampuni zimekuwa zikizingatia sana kuongeza uzalishaji ili kupunguza gharama na kupata idhini ya serikali kuuza bidhaa zao. Sasa, pia wanajaribu kujua jinsi ya kukabili upigaji marufuku wa bidhaa zao katika majimbo mbalimbali. Upside Foods ilianzisha mchakato kwenye mtandao wa Change.org kutafuta saini, ikialika wafuasi "kuwaambia wanasiasa waache kudhibiti chakula chako."

"Ni aibu wanaufunga mlango kabla hatujafunguliwa" alisema Tom Rossmeissl, mkuu wa masoko ya kimataifa wa Good Meat. Kampuni hiyo ambayo inafikiria hatua za kisheria, alisema.

Wanaounga mkono marufuku hizo wanasema wanataka kulinda wakulima na watumiaji. Wanasema nyama inayozalishwa maabara imekuwepo kwa karibu muongo mmoja tu, na wanahofia usalama wake.

"Wa-Alabama wanataka kujua wanachokula, na hatuna taarifa yoyote kuhusu kilicho ndani ya vitu hivi au jinsi kitakavyotuathiri," aliandika Seneta wa jimbo la Republican Jack Williams, aliyependekeza muswada wa Alabama, katika barua pepe kwa Associated Press. "Nyama inatoka kwa mifugo inayofugwa na wakulima na wafugaji wanaofanya kazi kwa bidii, si kutoka kwa sahani inayokuzwa na wanasayansi."

Lakini wale walio ndani ya sekta ya nyama inayozalishwa wanasema bidhaa zao lazima zipitie majaribio makali ya usalama wa serikali kabla ya kuuzwa. Sekta yao changa haijaribu kubadilisha nyama, wanasema, lakini kugundua njia za kukidhi mahitaji ya ulimwengu yanayoongezeka ya protini.

Rossmeissl alisema Marekani kwa sasa inaongoza jitihada za kukuza nyama na samaki zinazozalishwa maabara, ikiwa na kampuni 45 katika sekta hiyo, lakini hiyo inaweza kubadilika. Mwezi Januari, kwa mfano, kampuni moja ya Israeli ilipokea idhini ya awali ya kuuza steak za kwanza duniani zinazozalishwa kwa nyama ya ng'ombe inayozalishwa maabara. China pia inawekeza sana katika nyama inayozalishwa maabara.

Seneta wa jimbo la Jay Collins, Mrepublican aliyependekeza muswada wa Florida, alibainisha kwamba sheria hiyo haipigi marufuku utafiti, bali uzalishaji na uuzaji wa nyama inayozalishwa maabara. Collins alisema usalama ulikuwa kichocheo chake kikuu, lakini pia anataka kulinda kilimo cha Florida.

"Tusikimbilie kubadilisha vitu," alisema. "Ni sekta ya mabilioni ya dola. Tunawalisha watu wengi nchini kote kwa sekta zetu za ng'ombe, nyama ya nguruwe, kuku na samaki."

Rossmeissl anafikiria sekta ya nyama inajaribu kuepuka kile kilichotokea kwa sekta ya maziwa baada ya kuanzishwa kwa mbadala za mimea kama maziwa ya mtama. Maziwa ya mimea yalichukua asilimia 15 ya mauzo ya maziwa ya Marekani mwaka jana; hiyo ni kutoka karibu asilimia 6 muongo mmoja uliopita, kulingana na Idara ya Kilimo ya Marekani na Taasisi ya Chakula Bora, kikundi cha kutetea bidhaa za mimea na zinazozalishwa maabara.

Wazalishaji wa nyama waliunga mkono marufuku huko Florida na Alabama. Viongozi wa vyama vya wafugaji wa ng'ombe vya majimbo hayo - ambavyo ni vikundi vya kutetea wafugaji - walisimama pamoja na magavana wote wawili waliposaini marufuku hizo kuwa sheria.

Taaisi ya Nyama - inayowakilisha JBS, Tyson na kampuni zingine kubwa za nyama - ilituma barua kwa wabunge wa Alabama kuwaonya kwamba marufuku ya jimbo hilo inawezekana siyo ya kikatiba kwani sheria ya shirikisho inasimamia usindikaji wa nyama na biashara kati ya majimbo.

Waanzilishi wa Wildtype, kampuni iliyoko San Francisco inayozalisha samaki aina ya salmoni kwa njia ya maabara, walisafiri hadi Florida na Alabama kutoa ushahidi dhidi ya miswada hiyo lakini hawakuweza kushawishi matokeo. Wanatumaini mtu atapinga marufuku hizo mahakamani lakini wanasema si kweli kwa kampuni yao ndogo kuchukua vita hiyo.

-Imetayarishwa na Patrick Newman, VOA, Washington, D.C.

Forum

XS
SM
MD
LG