Habari zilisikika Alhamisi jioni kwamba Rais wa zamani Trump anashtakiwa na mwanasheria wa wilaya ya Manhattan Alvin Bragg, ingawaje mashtaka hayo bado hayajabainishwa wazi.
Mashtaka hayo hayatokani na shambulizi kwenye Bunge la Marekani lililofanywa na wafuasi wa Trump hapo Januari 6, 2021, ambapo Trump bado anaendelea kuchunguzwa,
Lakini kwa kumlipa mcheza filamu za ngono Stormy Daniels, ambaye anasema Trump alimuomba akae kimya kuhusu mahusiano yao ya kingono. Mwendesha mashtaka wa zamani wa serikali kuu Neamah Rahmani alisema kuwa dunia inaona historia ikijitokeza.
Neama Rahmani, Mwendesha Mashtaka wa Zamani anaeleza:“Hii ni mara ya kwanza kwa rais wa zamani kushtakiwa kwa uhalifu.”
Trump anawania tena urais mwaka 2024. Ameiita hatua hiyo ni mateso ya kisiasa na kuingilia kati uchaguzi, katika posti yao aliyobandika katika tovuti. Mark Funk mkazi wa Dallas, Texas anakiri kushtakiwa kwa Trump ni hatua iliyochukuliwa na maadui zake.
Mark Funk, Mkaazi wa Texas anasema: “Watajaribu kumuonyesha au kujaribu kumfanya aonekane kuwa si maarufu kadri wanavyoweza. Inaoneakana wamekuwa wakimfuatilia tangu aliposhinda uchaguzi wa kwanza.”
Mwanamke wa New York, hata hivyo, anakaribisha hatua hiyo ya kushtakiwa Trump.
Jennifer Cabana, Mkaazi wa New York anaeleza: “Nadhani ni habari ambayo taifa zima na dunia kwa jumla walikuwa wakiisubiri, kitu gani kitatokea katika kesi hii. Nadhani kama ni haki basi inahitaji kushughulikiwa, haijalishi wewe ni nani, haki inahitaji kushughulikiwa.”
Mchambuzi wa siasa Sherry Bebitch Jeffe anasema hatua ya mwendesha mashtaka Mdemocrat huenda ikamsaidia Trump na wafuasi wake ambao wakati anawania uteuzi wa Republican kuwania urais.
Jeffe, amesema: “Watakuwa wamekasirika. Hawatakubali ashtakiwe. Bado ni mapema mno, lakini kama ghadhabu itaendelea hadi kwenye uchaguzi wa awali, watajitokeza. Idadi ya wapiga kura watakaojitokeza itakuwa ni kubwa mno.”
Lakini anasema kushtakiwa kwake kutamuumiza Trump katika uchaguzi, kutamgharimu kura kutoka kwa wagombea huru. Anasema inaacha doa katika taifa.
Kushtakiwa hakutamsitisha Trump kuwania urais, na hata kushtakiwa, watalaamu wa kikatiba wanasema, huenda ikamzuia kuchukua uongozi kama akishinda.
Habari hii ina taarifa zinazotokana na vyanzo mbalimbali vya habari