Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:16

Mwinyi amteua Masoud kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar


Makamu wa Rais mteule Othman Masoud Othman
Makamu wa Rais mteule Othman Masoud Othman

Othman Masoud Othman ameteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, nafasi iliyo achwa wazi na Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alifariki dunia tarehe 17 Februari, 2021, Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Marehemu Seif Sharif Hamad
Marehemu Seif Sharif Hamad


Hatua hiyo imekuja baada ya chama cha ACT Wazalendo kukamilisha mchakato wa kupendekeza jina la atakaye rithi nafasi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar, Zena Said imesema Rais Mwinyi amezingatia kifungu cha 9(3) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Tamko la serikali ya Zanzibar
Tamko la serikali ya Zanzibar

Kifungu hicho kinasema, ‘Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na kutimiza lengo la kufikia demokrasia.’

Pia Rais wa Zanzibar, Mwinyi amepewa uwezo chini ya kifungu Namba 39(3) cha Katiba ya Zanzibar kufanya uteuzi huo.

“Baada ya kushauriana na Chama cha ACT-Wazalendo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Hussein Mwinyi amemteua Mheshimiwa Othman Masoud Othman Sharif kuwa Makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar,” imesema taarifa hiyo.

Kulingana na taarifa hiyo uteuzi huo unaanza Machi Mosi na sherehe za kumwapisha Masoud zitafanyika Jumanne Machi 2 katika ukumbi wa Ikulu ya Zanzibar.

Masoud amewahi kuhudumu katika nafasi za ngazi za juu katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo mwanasheria Mkuu wa Serikali na kwa sasa ni mwanachama wa ACT Wazalendo.

Kadhalika anatambuliwa kwa msimamo wake usioyumba wa kutetea maslahi ya Zanzibar ndani na nje ya nchi na pia uwezo wake mkubwa kwenye taaluma yake ya sheria.

XS
SM
MD
LG