Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 19:46

Matukio muhimu ya teknolojia mwaka 2020 na jinsi ilivyotumika 


App ya simu kufuatilia maambukizi ya COVID-19 ikianza kutumika Disemba 4, 2020, mjini Charlotte, Jimbo la North Carolina.
App ya simu kufuatilia maambukizi ya COVID-19 ikianza kutumika Disemba 4, 2020, mjini Charlotte, Jimbo la North Carolina.

Watu kote duniani waligeukia teknolojia, kuwasaidia kukabiliana na athari za janga la virusi vya Corona. 

Hata hivyo, wakati mwingine teknolojia hiyo haikuwa na mafanikio kama baadhi walivyotarajia.

Ripoti hii inaangazia hayo na mengine, kuhusu ripoti za sayansi na teknolojia zilizogonga vichwa vya habari ulimwenguni kote.

Watu wamegeukia teknolojia kuliko wakati mwingine wowote kabla ya janga la virusi vya Corona. Iwe ni kazi, masomo au hata kumuona daktari au kuwa karibu na jamaa na marafiki.

Kwa njia nyingi umekuwa ni mwaka ambao teknolojia imejitokeza kuonyesha jinsi inavyoweza kuwa na nafasi kubwa sana katika maisha ya binadamu.

Eric Ries ni mwandishi wa kitabu kiitwacho “The Lean Startup.” Anasema “hapana shaka kwamba mamilioni ya watu, teknolojia imeokoa maisha yao.”

Kutoka kitabu cha "Lean Startup Model "- Eric Ries. Photo Sachhoc.com
Kutoka kitabu cha "Lean Startup Model "- Eric Ries. Photo Sachhoc.com

Eric ni mjasiriamali mahiri ambaye hutoa hotuba mbalimbali kuhusu ubunifu. Mwanzoni mwa janga hili la Corona, alifurahi sana kuona makampuni ya teknolojia, wajasiriamali na wataalamu wa teknolojia wakijizatiti kuwasaidia watu.

Mwanzoni mwa mwaka, kampuni za Google na Apple ziliunda ushirikiano wa kihistoria, uliowawezesha watu kutumia simu zao za mkononi, kufahamu kama walikuwa wamepata virusi vya Corona au kama walikuwa wamekaribiana na watu waliokuwa wamepata maambukizi.

Lakini baadaye mradi huo ulikwama. App ya simu ya Smartphone, iliyobuniwa na kampuni ya Google kwa ushirikiano na ile ya Apple ilizinduliwa mapema mwezi huu wa Disemba.

Apps za mitandao ya kijamii
Apps za mitandao ya kijamii

“Inabidi tuseme kwamba juhudi hizo zote hazikufua dafu, kwasababu ilituchukua muda mrefu mno kukanza kuzitumia app hizo. Hebu fikiria, mwanzoni mwa janga hili, mtu alikuwa amesema tungefanikiwa kupata chanjo, hata kabla ya app hizo, kuanza kufanya kazi ipasavyo. Moja ni juhudi kubwa mno ya kisayansi, na nyingine ni rahisi kufanya,” anasema Erir Ries.

Eric anasema juhudi kama hizo zilikwamishwa na kutokuwa na uratibu unaofaa kutoka serikalini, kutokuwa na uelewa wa kutosha katika nyanja ya teknolojia, kuhusu ni nani anafanya maamuzi kwenye ngazi za chini, na jinsi ya kuwafikia walengwa.

Kameka Dempsey ni mwanachama wa jopokazi la Covid-19 ambalo liliundwa kwa minajili hiyo, kuwaunganisha wanateknolojia na serikali. Anasema ukosefu wa teknolojia ya kutosha umekuwa pigo kubwa katika vita vya kupambana na janga hilo.

"Kuna watu ambao wanaishi vijijini na hawana mtandao wa internet. Unaona... jambo kama watu kutoweza kutumia talakishi, simu za mkononi na kadhalika, ili kupata mafunzo, kufanya kazi, na kutekeleza majukumu mengine,” anasema Dempsey.

Anasema janga hili limewafanya watu wakatathmini upoya ni nini muhimu katika Nyanja ya teknolojia.

Dempsey anasema “kwasababu ya janga hili, teknolojia inawafanya watu kurejea ubunifu wa hali ya juu. Ubunifu ambao unatokana na haja kuu ya kutatu mzozo ambao unamkabili mtu, mwenye mahitaji.”

Matukio mengine katika mwaka 2020 umeshuhudiwa uzinduzi mkubwa wa mfumo wa mawasiliano wa 5G. Makampuni makubwa ya teknolojia ya simu kote duniani, yalizindua mifumo ya 5G kwenye simu mbalimbali.

Pia umeshuhudia kurejea kwa simu za mkononi za kujikunja, ambazo zilikuwa maarufu mnamo miaka ya 90, lakini tofauti na wakati huo, zilizotoka mwaka 2020 zimeongezewa teknolojia ya kisasa.

Mfano ni Samsung Galaxy Z Flip ambayo ilisifiwa na wachambuzi kama iliyokuwa imerekebisha hitilafu zote zilizokuwa kwenye simu za awali za Galaxy Fold na Galaxy Z Fold, zilizokuwa zimezinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2019.

Kwa upande wa kampuni ya Apple, ni mwaka ambao ilisitisha ushirikiano wake wa kibiashara na kampuni ya Intel na kuanza kujenga processor za komputa zake za Mac bila kuihusisha kampuni hiyo.

Hatua hiyo inatajwa na wataalam kama ambayo ni muhimu mno katika kuimarisha mfumo unaotumika kuunda talakilishi za macbook katika siku za usoni.

Mjasiriamali wa vifaa na vyombo vinavyotumia teknolojia ya hali ya juu Elon Musk, anatajwa na shirika la habari la Reuters kama ambaye ameongeza utajiri wake maradufu mwaka 2020 licha ya janga la virusi vya Corona.

Gari muundo wa Tesla, liliendelea kupata umaarufu mkubwa, hususan kwa matajiri wakubwa duniani, licha ya kwamba kampuni hiyo ya musk iliuza idadi ndogo tu ya magari hayo.

Musk sasa anashikilia nambari ya pili kwa watu matajiri sana duniani, nafasi ya kwanza ikishikiliwa na mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Amazon, inayouza bidhaa kwa njia ya mtandao, Jeff Bezos.

Musk pia amekuwa gumzo katika ngazi ya teknolojia za anga za juu kwani serikali ya Marekani ilishirikiana na kampuni yake ya SpaceX, na kutuma vyombo kadhaa kwenda anga za juu.

Ni mwaka ambao pia umeshuhudia udukuzi wa akaunti za mitandao ya kijamii za watu mashuhuri duniani, ikiwa ni pamoja Ellon Musk, mfanyabiashara bilionea, Bill Gates, na rais wa zamani wa Marekani Barack Obama.

Katika miezi ya mwisho ya mwaka 2020, pia idara za serikali ya Marekani zililengwa na wadukuzi, ambao utawala wa Trump na wataalam mbalimbali wanasema ulifanywa na wahalifu kutoka Russia.

Mwaka huo pia umekuwa na msukumo mpya wa uwajibikaji kwa makampuni ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Google na Twitter, kuwajibika zaidi, na kusaidia kupunguza uhasama na habari potovu.

Viongozi wa makampuni hayo walifika mbele ya kamati za bunge la Marekani kutoa maelezo kuhusu masuala yaliyozua utata.

Suala la habari za kupotosha linaendelea kuwa changamoto kubwa siyo tu katika nchi zilizoendelea, bali pia kwa nchi zinazoendelea.

Droni zinazotumika kumwagilia dawa mashambani na mbugani
Droni zinazotumika kumwagilia dawa mashambani na mbugani

Barani Afrika teknolojia iliyoimarishwa ya droni, imekuwa ya manufaa kwa wengi hususan katika nyanja ya usafirishaji wa vifaa vya kitabibu na dawa za kupambana na maambukizi ya Corona. Kisiwani Zanzibar, droni za kisasa zimetumika kwa wingi kunyunyizia dawa za kuwaua mbu katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa Malaria.

Ongezeko la michezo ya komputa pia limeshuhudiwa huku makampuni yanayotengeneza mifumo ya michezo hiyo kama Xbox yakiripoti kutokuwa na vifaa hivyo kwa sababu ya kununuliwa kwa wingi. Wataalam wanasema hii ilitokana na watu kukaa nyumbani wakizingatia masharti ya kupambana na maambukizi.

Silicon Valley, kitovu cha teknolojia nchini Marekani imejifunza mengi katika kukabiliana na janga hili. Lakini sasa kinachosalia ni kuona jinsi itakavyotumia mafunzo hayo katika mwakaz 2021.

Imetayarishwa na mwandishi wetu BMJ Muriithi, Washington, DC.

Imetayarishwa na

XS
SM
MD
LG