Kulingana na taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Wako, pamoja na mkewe Flora Ngaira na mwanawe Julius Wako, wamepigwa marufuku kuingia Marekani.
Serikali ya Marekani inasema hatua hiyo imechukuliwa kutuma ujumbe kwamba Marekani inashirikiana na Kenya katika kupambana na rushwa.
Hata hivyo, taarifa hiyo haijaelezea waziwazi ni vitendo gani vya rushwa Wako alihusika navyo.
Wako alikuwa mwanasheria mkuu wa Kenya kwa muda wa miaka 20, kati ya mwaka 1991 na 2011.
Amos Wako kwa sasa ni seneta wa Kaunti ya Busia, magharibi mwa Kenya na vyombo vya habari vya Kenya vimemhusisha na nia ya kutaka kugombea nafasi ya gavana katika Kaunti hiyo.