Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:08

Miungano ya kisiasa katika Uchaguzi Mkuu Kenya 2022


FILE - Jomo Kenyatta, leader of the Kenya African National Union, gestures with his fist as he speaks in Nairobi, Kenya, in 1962.
FILE - Jomo Kenyatta, leader of the Kenya African National Union, gestures with his fist as he speaks in Nairobi, Kenya, in 1962.

Katika mfululizo wa makala yetu kuhusu uchaguzi wa Kenya, leo tunaangazia miungano ya kisiasa, baina ya vyama mbalimbali, baadhi vikiwa na itikadi au sera zinazowiana, na vingine vikiungana kwa kila kinachoelezwa kama  sababu ya kutafuta uongozi wa kisiasa tu.

Tutalenga historia ya miungano hiyo, mafanikio, na changamoto ambazo zimekuwepo kwa miongo kadhaa. Na licha ya bunge la nchi hiyo, kuweka msingi wa kisheria, kuilinda miungano kama hiyo, mapema mwaka huu, wachambuzi wanasema, matatizo bado yameendelea kuwepo.

Miungano ya kisiasa nchini Kenya, imekuwepo tangu miaka ya hamsini, hata kabla ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa Uingereza.

please wait

No media source currently available

0:00 0:10:56 0:00

Kabla ya mwaka wa 1963, chama cha Kenya African National Union (KANU) kilichotawala kwa takriban miaka 40 baada ya Kenya kupata uhuru mwaka 1963 hadi kushindwa katika uchaguzi wa 2002, Kilijulikana kama Kenya African Union (KAU), lakini kikaungana na chama cha Kenya Independent Movement, chake marehemu Tom Mboya, hapo mwaka wa 1960, na kubadilishwa jina chini ya makubaliano ya muungano huo.

Baada ya hapo, hakukuwa na upinzani mkali kwa KANU, na wala utawala wa rais wa wakati huo Jomo Kenyatta, haukuona haja ya kubadilisha sheria na kuwa na mfumo wa chama kimoja. Lakini hali hiyo ilibadilika chini ya utawala wa Rais Daniel Arap Moi, aliyechukua usukani kama kiongozi wa Kenya kufuatia kifo cha Rais Kenyatta hapo mwaka wa 1978, hususan baada ya jaribio la mapinduzi la mwaka 1982, ambapo bunge lilibadilisha sheria na kuzuia kuwepo vyama vingi vya kisiasa, bila idadi kubwa ya Wakenya kushirikishwa katika hatua hiyo.

Hayati Rais wa zamani Daniel Arap Moi
Hayati Rais wa zamani Daniel Arap Moi

Lakini ni mwanzoni mwa miaka ya tisini, ambapo mfumo wa vyama vingi vya kisiasa ulirejea.

Baada ya Rais Moi, na chama kilichokuwa kikitawala cha KANU kuridhia kufanyia marekebisho kipengele cha katiba ya zamani cha 2A hapo mwaka wa 1991, ambacho kilikuwa kimeifanya Kenya kuwa ya mfumo wa chama kimoja, taswira ya siasa za taifa hilo ilibadilika ghafla.

Vyama vya upinzani vilianza kuchipuka, kila kimoja kikiamini kwamba kingeuondoa utawala wa Kanu Madarakani.

Lakini kutokana na mbinu zilizotumiwa na Rais Moi na wandani wake, haikuchukua muda mrefu kabla ya wanasiasa wa upinzani kugundua kwamba haingekuwa rahisi kukishinda chama hicho, ambacho kilikuwa kimeongoza, siyo tu tangu mwaka wa 1982, wakati bunge lilipofanyia marekebisho katiba na kuifanya nchi hiyo kuwa ya mfumo wa chama kimoja, lakini miongo miwili kabla ya hapo.

Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1992, ambapo Kanu ilishinda licha ya msisimko mkubwa kwa kisiasa kushuhudiwa, baadhi ya wanasiasa wa upinzani walianza kubadilisha mikakati yao ya kisisa. Pamoja na vyama, vuguvugu za kila aina zilizundwa, huku kila moja likitumai kwamba lingefaulu katika azma ya kumuondoa rais Moi madarani.

Lakini bado, hawakukubaliana kwa kauli moja kuhusu namna ya kukabiliana na KANU. Na hapo mwaka wa 1997, Moi na KANU, walishinda uchaguzi mkuu kwa mara nyingine. Mchambuzi wa siasa za Kenya Bi Mainuna mwidau, anatupia jicho hali ilivyokuwa wakati huo.

Lakini licha ya kutokuwepo na mikakati madhubuti ya miungano ya kisisasa iliyolindwa kisheria, wanasiasa wa upinzani wa wakati huo walifanikiwa kuja pamoja na kushinda uchaguzi wa mwaka 2002, uliomwingiza madarakani Rais Mwai Kibaki.

Lakini kilichofuatia ushindi huo ni mgawanyiko mkubwa serikalini, uliopelekea Rais Mwai Kibaki kulivunja baraza nala mawaziri n ahata kuwafuta wengi wao, baada ya kushindwa katiak kura ya maambuzi kuhusu kubadilisha katiba iliyofanyika mwaka wa 2005. Tumemuuliza Maimuna Mwidau, ni kwa nini licha ya muungano wa NARC kuunda serikali, bado changamoto zilionekana kuongezeka.

Hayati Rais wa zamani Mwai Kibaki
Hayati Rais wa zamani Mwai Kibaki

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ulioibua utata na kupelekea vifo vya Zaidi ya watu 1200, serikali ya muungano iliundwa, ikiitwa ya Umoja wa kitaifa. Nayo iligubikwa na changamoto chungu nzima, hususan kwa sababu walioiunda hawakuwa na msimamo mmoja wa kisera.

Ingawa katiba mpya ya mwaka wa 2010, ilibadilisha mwelekeo wa siasa za Kenya kwa njia mbalimbali, baadhi ya wachambuzi wanasema iliifanya hata vigumu zaidi kwa chama kimoja cha kisiasa kuunda seriali bila kushirikisha vingine.

Katiba hiyo ilionekana kuongeza hali ya sintofahamu kwa walionuia kuunda miungano huku ikiwaacha wanasiasa bila ya linguine, ila kushirikiana na watau ambao, kabala ya hapo, walikuwa mahasimu wao wa kisiasa.

Licha ya kwamba chama cha PNU na kile cha URP vilikuja pamoja na kuunda serikali mwaka wa 2013, baadaye mgawanyiko ulishuhudiwa ndani ya serikali hiyo, na kufikia mwaka wa 2016 ambapo vyama vingi viliungana na kuunda chama kimoja cha Jubilee, sio wote walioridhia.

Baadaye, Jubilee iligawanyika na kuwa mirengo miwili ya kisiasa.

Kwa upande mwingine, miungano iliyoundwa na vyama vya upinzani kwelekea kwa uchaguzi wa mwaka 2013 na 2017, ikijulikana nkama CORD na NASA mtawalia, hatimaye ilisambaratika, kutokana na kile baadhi ya wachambuzi walisema ni kutoaminiana kwa viongozi, na kukosa uungwaji mkono wa kisheria kwa mikataba iliyotiwa saini.

Lakini hilo halikuwafanya Wakenya kuachana na miungano ya kisiasa. Mapema mwaka huu, bunge lilipitisha sheria zilizoibua utata ambazo zinaipatia nguvu miungano hiyo, na kuplekea hali iliyoko kwa sasa ambapo kiongozi wa ODM, Raila Odinga anapeperusha bendera ya Muungano wa Azimiao la Umoja One Kenya, huku mpinzani wake mkuu, William Ruto, akiwa mgobea kwa tikiti ya chama cha UDA, chini ya muungano wa Kenya Kwanza. Miungano yote miwili imeunda na vyama mbalimbali.

KENYA : William Ruto na Raila Odinga
KENYA : William Ruto na Raila Odinga

Pamoja na kuwepo na sheria inayoratibu miungano ya kisiasa, taifa hilo la Afrika Mashariki bado limeendelea kukabiliana na changamoto za hesabu ya kikabila, mifumo dhaifu ya vyama na ukosefu wa uaminifu kuhusu maudhui ya mikataba iliyotiwa saini. Je, miungano hii inaashiria nini kwa mstakabali wa siasa za Kenya. Kevin Osido ni mchambuzi wa siasa za Kenya na mtaalam wa masuala ya uongozi.

Kwa sasa, historia ndiyo itakayoamua iwapo hatua ya kuunda sheria ya kuwezesha vyama mbalimbali kuungana kwa madhumuni ya kuunda serikali, itakuwa na matokeo chanya kwa taifa au la.

Imetayarishwa na mwandishi wetu BMJ Muriithi Washington, DC.

XS
SM
MD
LG