Katika hafla maalum iliyofanyika katika Kasri ya Mfalme huko Tokyo, Naruhito alikubali kupokea alama za utawala wa ufalme ikiwa ni pamoja na upanga na jiwe la thamani na muhuri wa taifa pamoja na muhuri wake binafsi.
Hotuba yake fupi mara baada ya kupokea utambulisho wa ufalme, mfalme huyo mpya amesema anaunyekevuvu na heshima kubwa kupewa madaraka hayo na kuahidi kufuata nyayo za baba yake, Akihito, aliyeachia madaraka siku moja kabla.
Mke wa mfalme, Malkia Masako, alikuwa pembeni yake wakati akitoa hotuba hiyo, lakini alikuwa amezuiliwa kuhudhuria sehemu ya kwanza ya tafrija kutokana na utamaduni wa muda mrefu ambao unaruhusu wanaume tu katika familia ya kifalme kuhudhuria.
Naruhito anakuwa mfalme wa Japan wa 126 baada ya saa sita usiku Jumatano.
Mfalme Emeritus Akihito mwenye umri wa miaka 85, mara ya kwanza alitangaza mpango wa kuachia madaraka mwaka 2016, akieleza wasiwasi wake juu ya umri aliofikia na changamoto za kiafya katika kutekeleza majukumu yake.
Mfalme huyo wa Japan aliyeachia madaraka aliingia kutawala Januari 1989 baada ya kifo cha baba yake, ambaye ni Mfalme wa kipindi cha Vita Dunia II Hirohito, ni wa kwanza kuachia madaraka katika kipindi cha miaka 200.