Magavana kutoka mataifa yote mawili walitembelea kaskazini mwa Cameroon Ijumaa baada ya kufanya mkutano wa dharura mjiji Diffa Niger. Wanasema kwamba mamilioni ya watu wakiwemo waliotorikea ghasia kati ya wakulima, wavuvi na wafugaji, na wanaorejea makwao wanahitaji misaada ya chakula pamoja na usaidizi wa makazi.
Maafisa kutoka halimashauri ya ziwa Chad wanasema kwamba mamilioni ya wakimbizi pamoja na watu waliokoseshwa makazi wanaorejea kwenye miji na vijiji vya Cameroon, Chad, Nigeria na Niger wanahitaji misaada ya dharura ili kuokoa maisha.
Kundi la kigaidi la Boko Haram kwenye maeneo hayo limeacha zaidi ya watu 36,000 wakiwa wamekufa hasa nchini Nigeria , wakati takriban milioni 3 wakilazimika kutoroka makwao, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa.
Midjiyawa Bakari ni mwenyekiti wa halimashauri hiyo inayojumuisha magavana wanane kutoka majimbo yalioathiriwa na Boko Haram.
Anasema kwamba alitembelea majimbo hayo nchini Niger na Cameroon mwishoni mwa wiki, ili kujionea mwenyewe changamoto wanazopita wale wanaorejea kwenye miji na vijiji vyao.
Bakari alizungumza na chombo cha habari cha Niger cha Tele Sahel pamoja na chombo cha habari cha serikali ya Cameroon cha CRTV.
"Migogoro kadhaa imeripotiwa miongoni mwa watu wanorejea kwenye maeneo yanayozunguka ziwa Chad, ambako ni nyumbani mwa takriban watu milioni 40. Ziwa hilo limepungua kwa asilimia 60 katika ndani ya miaka 60 iliyopita. Bakari anasema kwamba wakazi wa eneo hilo wanategemea ufugaji, uvuvi na ukulima. Anasema kwamba wamefanya mkutano wa dharura na Mohamed Mouddour ambaye ni gavana wa jimbo la Diffa, ili kujionea namna maisha ya mamilioni ya watu yalivyoathiriwa na namna yanavyoweza kuimarishwa, pamoja na kuhakikisha usalama wao dhidi ya mashambulizi kutoka kundi la Boko Haram," alisema.
Bakari ambaye pia ni gavana wa jimbo la kaskazini mwa Cameroon la Far North karibu na mpaka wa Chad na Nigeria analaumu mabadiliko ya hali ya hewa kwa kupungua kwa maji ya ziwa Chad. Anasema kwamba mizozo kati ya wafugaji, wavuvi na wakulima kutokana na uhaba wa maji inaripotiwa kila wiki.
Kundi lao linasema kwamba maelfu ya watu waliolazimika kuondoka makwao mwaka jana kutokana na mafuriko pamoja na mashambulizi ya ndovu wanahitaji misaada ya kuwasidia kupata makazi.
Wakati magavana wakiomba misaada ya kimataifa kwa wakimbizi wanaorejea au kukoseshwa makazi Cameroon, Nigeria na Chad, ripoti zinasema kwamba wadudu pamoja na ndege wameshambulia maelfu ya hektari za chakula kwenye mashamba yao. Mashamba hayo yanamilikiwa na watu waliotoroshwa makwao au yale yaliopandwa chakula kwa ajili ya wakimbizi na watu waliokoseshwa makazi.
Jean Felix Wankague ambaye ni afisa wa kilimo na ufugaji mwenye gazi ya juu zaidi kwenye ofisi za serikali ya Cameroon iliyoko kwenye mpaka wa kaskazini karibu na Chad na Nigeria ameambia VOA kwa njia ya ujumbe wa mtandao wa Whats app kwamba wadudu na ndege wameharibu mamia ya mashamba yam tama, mpunga na mahindi.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu OCHA inasema kwamba mwaka huu, mamilioni ya watu walioathiriwa magharibi na kati mwa Afrika watabaki kwenye hali tete kutokana na kutokuwepo misaada ya kibinadamu ya kutosha.
OCHA inasema kwamba dola bilioni 2.53 zinahitajika ili kukabiliana na mzozo wa kibinadamu uliopo katika kusaidia takriban watu milioni 7.4