Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 06:58

Kimbunga Ian: Wakazi wa Florida waharakisha kununua bidhaa na kuhamia sehemu salama


Wasafiri wakijaribu kubadilisha safari zao kufuatia kimbunga Ian, katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Tocumen, Panama City, Sept. 27, 2022.
Wasafiri wakijaribu kubadilisha safari zao kufuatia kimbunga Ian, katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Tocumen, Panama City, Sept. 27, 2022.

Wakazi wa pwani Florida kwenye Ghuba ya Mexico, wameharakisha kununua bidhaa muhimu na chakula kwenye maduka huku wakiondoka na wengine kuhamia kwenye makazi ya muda wakati kimbunga Ian kikikaribia hii leo.

Kimbunga kinachoelekea Florida kinatarajiwa kuwasili kwenye Ghuba hiyo Jumatano usiku huku tahadhari ikiendelea kutolewa kwa wakazi kuondoka na kuhamia kwenye makazi ya muda.

Kimbunga Ian kinazidi kupata nguvu na kuwa kimbunga hatari sana cha kiwango cha 4, kituo cha kitaifa cha vimbunga marekani NHC kilisema Jumatano.

Wakazi wa Florida walichukua hatua za haraka kuondoka majumbani mwao kwa dharura, baadhi wakificha mali zao za thamani kwenye ghorofa za juu na kukimbia wakihofia dhoruba hiyo mbaya inayotarajiwa kupiga pwani ya magharibi ya jimbo lao baadaye hii leo.

Wakazi wa Florida wakijiandaa kukabiliana na Kimbunga Ian wakati kikiwa kiko njiani kuelekea upande wa magharibi ya jimbo hilo, Jumanne, Septemba 27, 2022, huko Tampa, Fla.
Wakazi wa Florida wakijiandaa kukabiliana na Kimbunga Ian wakati kikiwa kiko njiani kuelekea upande wa magharibi ya jimbo hilo, Jumanne, Septemba 27, 2022, huko Tampa, Fla.

Renee Correa, mkazi wa Tampa anaeleza: "Nimeishi hapa kwa miaka 45, na hii ndio mara yangu ya kwanza kuondoka kwa sababu ya dhoruba. Maji yananitisha sana. Ilinichanganya sana na sikutaka kuhatarisha maisha yangu, kwa hivyo niliondoka na mbwa wangu na binti zangu, ni dhoruba ya kutisha."

"Ni dhoruba kubwa, itakayoleta maji mengi itakapowasili," Gavana wa Florida Ron DeSantis aliuambia mkutano wa waandishi wa habari katika mji mkuu wa Florida huko Sarasota, mji wa pwani wa watu 57,000 uliopo katika njia inayotarajiwa ya dhoruba.

Yeye alionya "Hii ndiyo aina ya dharuba inayosababisha mawimbi makubwa inayotishia maisha."

Gavana Ron DeSantis, (R) Florida asema: "Unapoangalia mawimbi makubwa kutokana na dhoruba ya aina hii, ni hatari inayotishia maisha. Unapozungumzia futi kumi, futi 12 za mawimbi ya dhoruba, ambayo unaweza kuona katika baadhi ya sehemu itakapofika kwenye nchi kavu"

Kimbunga Ian kilipita magharibi mwa Cuba siku ya Jumanne kama kimbunga cha kiwango cha 4 kabla ya kuelekea Florida, ambapo maafisa wamewaamuru watu milioni 2.5 kuhama kabla ya kufika hii leo.

Kimbunga kilifika majira ya saa 10 na nusu usiku Jumanne katika mkoa wa Pinar del Rio wa Cuba, ambako maafisa waliweka makazi ya muda yapatayo 55 na kuhamisha watu 50,000 huku wakichukua hatua kulinda zao muhimu la nchi hiyo la tumbaku linalopatikana zaidi sehemu hiyo ya nchi.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Karine Jean-Pierre alisema idara ya huduma za dharura ya Marekani FEMA iko tayari kutoa msaada huko Florida.

Karine Jean-Pierre, Msemaji wa Ikulu ya Marekani: "Mwishoni mwa juma, rais aliidhinisha ombi la msaada wa dharura kutoka Florida mara tu alipolipokea na kuelekeza timu yake kuharakisha msaada wa serikali katika jimbo hilo kabla ya kimbunga kufika. FEMA imeweka tayari vifaa katika maeneo ya muhimu huko Florida na pia Alabama. Inajumuisha majenereta, chakula na mamilioni ya lita za maji.

Ukanda wa pwani wa Florida ambao uko katika hatari hii ya kimbunga ni eneo lenye fukwe nzuri za mchanga, hoteli nyingi za mapumziko zinazopendwa na wastaafu na watalii.

Mashirika ya ndege yaliripoti kusitisha safari za ndege zaidi ya 2,000 kutokana na kimbunga huku viwanja vya Ndege vya Kimataifa vya St. Petersburg-Clearwater na Tampa vimefungwa tangu Jumanne.

XS
SM
MD
LG