Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 00:58

Kampuni ya Taifa Gas ya Tanzania kujenga kiwanda cha gesi nchini Kenya


Wanawake wameketi wakipika katika kitongoji duni cha Kibera kilichopo katika mji mkuu wa Nairobi, Kenya Juni 8, 2009. Picha na shirika la habari la REUTERS/Noor Khamis (KENYA SOCIETY).
Wanawake wameketi wakipika katika kitongoji duni cha Kibera kilichopo katika mji mkuu wa Nairobi, Kenya Juni 8, 2009. Picha na shirika la habari la REUTERS/Noor Khamis (KENYA SOCIETY).

Kampuni ya gesi ya kupikia, Taifa Gas, kutoka Tanzania, imeanzisha rasmi ujenzi wa kiwanda na ghala ya kuhifadhi gesi ya kupikia ya tani elfu 45, katika eneo maalumu la kiuchumi, barabara ya Dongo Kundu, karibu na bandari ya Mombasa, Kenya.

Kiwanda hicho cha mabilioni ya fedha kitagharimu dola milioni 200.

Taifa Gas itatoa ushindani wa kibiashara na kampuni ya Africa Gas and Oil Limited (AGOL) yenye kiwanda cha tani elfu 25, kinachomilikiwa na Mohammed Jaffar, Mombasa.

Akizindua rasmi ujenzi huo kwa kuweka jiwe la msingi, rais William Ruto wa Kenya, amesema kama serikali wanaunga mkono mradi huo ambao sio tu kwa manufaa ya Kenya bali kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mbali na nafasi za ajira na kuinua uchumi, pia utachangia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kwa kupunguza utumiaji wa kuni na makaa kwa kupikia na badala yake kutumia nishati safi isiyoharibu mazingira.

“Asilimia 70 ya wakenya wanatumia kuni na makaa kwa upishi, hii sio tu kuwadhuru afya yao bali pia inachangia uharibifu wa misitu. Uzalishaji wa gesi safi utawasaidia wakenya kupata gas kwa bei nafuu na mazingira salama,” amesema Rais William Ruto.

Rais Ruto amesema kuwa uzinduzi wa kiwanda hicho ni wa kihistoria, na kwamba kinawiana na ruwaza ya taifa hilo ya kufikia nishati safi ifikapo mwaka 2030.

Mwenyekiti wa kampuni ya Taifa Gas, Rostam Aziz, ameipongeza serikali ya Kenya kukubali kuwekeza katika taifa hilo amesema kuwa awali alikuwa amelenga kujenga kiwanda na ghala ya kuhifadhi tani elfu 30 lakini rais akaongeza hadi tani elfu 45.

Azizi asema kuwa Dar es Salaam itakua makao makuu ya Taifa Gas, ambayo inasambaa katika mataifa mengine bara la Afrika.

“Tayari tumefungua afisi ya kampuni ya Taifa Gas nchini Rwanda na tutaendelea hadi Uganda, Burundi, Malawi, Zambia, Sudan Kusini na Afrika Kusini na tutaendelea hadi Djibouti na chi zote ambazo zinategemea bandari ya Mombasa. Tutahakikisha zitakuwa na Taifa Gas, na tutsambaza kutoka vijijini hadi mjini na itakua kampuni ya kwanza kutoka Tanzania kusambaa katika bara zima la Afrika katika miaka mitano.” amesema Rostam Aziz, mwenyekiti wa Taifa Gas.

Akigusia vikwazo vya uwekezaji katika mataifa ya Afrika, Aziz amewasihi marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuondoa kodi na vikwazo mipakani ili kutoa fursa kwa wawekezaji kuwa huru kuwekeza katika bara lao badala ya kutoa mwanya kwa mataifa kama China kuwekeza kwa urahisi na kuwawekea vikwazo wa Afrika wenyewe.

Kiwanda hicho cha Taifa Gas kitachukua miezi 15 kukamilika na kinatarajiwa kutoa nafasi elfu 90 za ajira.

Wenyeji wa eneo kunakotekelezwa mradi walipongeza uwekezaji huo kwamba utawapa nafasi za ajira na upatikanaji wa nishati safi, wameitaka serikali kuhakikisha wanawapa fidia kwa kufurushwa kwenye ardhi zao ili kutoa nafasi ya ujenzi wa kiwanda hicho.

XS
SM
MD
LG