Foleni kubwa ya watu wanaotaka kuuaga mwili wa hayati Malkia Elizabeth ilifungwa kwa muda Ijumaa baada ya watu kuwa wengi sana kuvuka uwezo wa mamlaka ya usalama kuweza kudhibiti.
Maafisa wa serikali walichukua hatua hiyo huku wakiwatahadharisha watu kwamba muda wa kusubiri ni mrefu na kufikia angalau saa 14.
Malkia Elizabeth alifariki Scotland akiwa na umri wa miaka 96 na kusababisha hisia nyingi zilizowaleta pamoja maelfu ya watu kushuhudia jeneza na kuuaga mwili wake mjini London.
Lango la kuingia kwenye mstari huo lilifungwa kwa muda kwa angalau saa sita, idara ya utamaduni ya Uingereza ilisema katika mtandao wake wa Twiter. Iliandika “ tafadhali usijaribu kuingia kwenye mstari hadi utakapofunguliwa.”
Foleni ndefu inatoka uwanja wa Southwark Park hadi ukumbi wa Bunge wa Westminster ambapo takriban watu 750,000 kwa jumla wanatarajiwa kupita mbele ya jeneza la Malkia kabla ya Jumatatu asubuhi siku ya maziko yake.
Foleni ilikuwa na urefu wa hadi maili 4.6 mtandao wa ufuatiliaji wa idara ya utamaduni umeonyesha.
Mmoja kati ya waombolezaji kutoka London, Naomi Brown amesema amesubiri kwa karibu saa 11 baada ya kujiunga kwenye foleni jana usiku baada ya kutoka kazini.