Awali, gari lililobeba mwili wa hayati Elizabeth, likiwa na maafisa wa kifalme na walinda usalama, liliondoka kwenye Kasri la Balmoral, muda mfupi kabla ya Jumapili adhuhuri, ukiwa ni mwanzo wa safari ndefu na ya mwisho, ya Malikia Elizabeth, aliyeaga dunia Alhamisi wiki jana, baada ya kushikilia wadhifa wa ufalme wa Uingereza kwa miongo saba.
Msafara wake ulionekana, kwa polepole ukipitia mabonde na milima ya Scotland, na mandhari iliyothaminiwa na marehemu , eneo ambapo alitumia wiki zake za mwisho za amani.
Katika miaka ya nyuma, malkia alionekana mara kwa mara akitembelea vijiji hivi vya mbali, alipokuwa akiishi katika Kasri la Balmoral, makao ambayo aliyapenda.
Wakazi walikusanyika kando ya barabara ili kumtazama kwa mara ya mwisho na kusema kwaheri.
Wengine alitulia na kuonyesha ukimya ambao ulikuwa ni ishara ya mshtuko ambao raia wa Uingereza walipata - na heshima ambayo marehemu Malikia alipewa wakati wa uhai wake.
Baadhi ya watu walirusha maua, huku wengine wakipiga vigelegele wakati gari la kubebea maiti lilipopita.
Wengi katika umati wa watu walibubujikwa na machozi.