Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 17:55

EU yamtambua Juan Guaido kama rais wa Venezuela


Kiongozi wa upinzani wa Venezuela, Juan Guaido, ambaye amejitangaza kuwa rais na kuungwa mkono na Umoja wa Ulaya na Marekani, kati ya wengine.
Kiongozi wa upinzani wa Venezuela, Juan Guaido, ambaye amejitangaza kuwa rais na kuungwa mkono na Umoja wa Ulaya na Marekani, kati ya wengine.

Mgogoro wa kisiasa unaoendelea kuikabili Venezuela ulichukuwa sura mpya Alhamisi baada ya bunge la Umoja wa Ulaya kutangaza kwamba linamtambuwa rasmi Juan Guaido wa Venezuela, kama rais wa muda wa nchi hiyo.

Wajumbe 429 walipiga kura kuunga mkono hatua hiyo wakati wa kikao maalum mjini Brussels, Ubelgiji.

Bunge hilo limesema litaendelea kumtambua Guaido kama kiongozi wa Venezuela hadi pale nchi hiyo itakapofanya uchaguzi huru na wa haki.

Hatua hiyo, inaendelea kuongeza changamoto zinazomkabili rais Maduro anayeegemea mrengo wa Kisocialisti, na ambaye anakabiliwa na mzozo mkubwa wa kisiasa tangu uchaguzi ulioibua utata mwaka jana.

Marekani na baadhi ya washirika wake wa ulaya, zimetangaza pia zinamtambua Guaido, ambaye alikuwa kiongozi wa bunge la nchi hiyo, kama kaimu rais, hatua ambayo imepingwa vikali na Russia, China na Uturuki, kati ya nchi zingine, ambazo viongozi wao ni washirka wa karibu wa Nicholas Maduro.

Wakati huo huo, chama cha waandishi wa habari chenye makao makuu mjini Brussels kimesema kuwa waandishi saba wa habari wameshikiliwa nchini Venezuela.

Umoja wa ulaya umeutaka utawala wa Maduro kuwaachilia huru.

Na huku Venezuela ikiendelea kukabiliwa na migogoro ya kiuchumi na kisiasa, Umoja wa ulaya tayari umeiwekea nchi hiyo vikwazo vya silaha na pia vya kibiashara, kuwazuia baadhi ya maafisa wa serikali ya Maduro kushirikiana kwa vyovyote vile na nchi wanachama wa muungano huo wa EU.

XS
SM
MD
LG