Wajumbe wa pande zote mbili wanaendelea na mazungumzo yao leo kwa siku ya tatu mfululizo mjini Bamako ikisemekana wanajeshi wanataka kubaki madarakani kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mazungumzo yanaendelea Jumatatu, pande hizo zimewaambia waandishi wa habari.
Viongozi wa kijeshi wanaongozwa na Kanali Assimi Goita na wasuluhishi wa ECOWAS wanaongozwa na Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan walikutana jana katika kikao cha faragha.
Msemaji wa kundi la wanajeshi kanali Ismael Wague nae amesema wamekubaliana kuhusu baadhi ya maswala na mashauriano zaidi yataendelea.
Maswala nyeti yanazongumziwa ni pamoja na hatma ya rais aliyeondolewa madarakani Ibrahim Boubacar Keita na maelezo kuhusu utawala wa mpito kukabidhi madaraka kwa serekali ya kiraia.
Radio Ufaransa RFI, Jumapili usiku ilisema kundi la kijeshi limependeleza serikali ya mpito ya miaka mitatu inayongozwa na mwanajeshi na ambayo inaundwa na wanajeshi wengi.
Taarifa hiyo ya RFI imeongeza kuwa wanajeshi wako tayari kumuruhusu Keita kurudi nyumbani kwake au kuondoka nchini.