Wizara ya mambo ya nje imetangaza kuwa ubalozi huo ulifunga milango yake saa nne asubuhi (0200GMT) majira ya eneo hilo, muda kama huo mamlaka nchini China ziliamuru ubalozi wa Marekani kufungwa na mara tu baada ya bendera ya Marekani kuteremshwa kwa mara ya mwisho. Dakika chache baadae, kundi la maafisa wa China waliingia katika jengo hilo na kuliweka chini ya himaya yao.
Ubalozi wa China mjini Beijing uliiaga ofisi yao ya Chengdu katika picha ya video iliyopostiwa baadae kwenye akaunti ya Twitter ya ubalozi huo, ikisema “tutakukosa daima.”
Kabla ya kufungwa, kulikuwepo na ulinzi mkali katika eneo la ubalozi huo mdogo Jumapili wakati wafanyakazi walikuwa wanajitayarisha kuondoka katika jengo hilo.
Malori matatu yalionekana yakiingia katika eneo la jengo hilo, wakati maaskari waliovalia sare za jeshi la polisi na wale waliovaa kiraia walijipanga pande zote mbili za barabara, zilizokuwa zimewekewa vizuizi vya chuma.
China imewashutumu baadhi ya wafanyakazi wa ubalozi mdogo hapo Chengdu kuwa walikuwa wanajishughulisha na mambo ambayo hayalingani na hadhi yao ya kidiplomasia.”
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbin alisema vitendo kama hivyo vilikuwa vinaingiliana na masuala ya ndani ya China na yameathiri maslahi ya usalama wake bila ya kutoa maelezo zaidi.
Amri ya kufunga ubalozi mdogo wa Marekani mjini Chengdu ilitolewa Ijumaa iliyopita kulipiza kisasi dhidi ya amri ya serikali ya Marekani iliyofunga Ubalozi mdogo wa China mjini Houston, Texas
Washington iliamrisha China kufunga ofisi ya Houston “kulinda haki miliki za kielimu na taarifa binafsi za Wamarekani.”
Wakati ubalozi mdogo wa China ukifungwa Ijumaa iliyopita, kundi la wanaume ambao walidaiwa kuwa ni maafisa wa Marekani walionekana wakivunja mlango wa nyuma kuingia katika jengo hilo.
Wang amesema Jumamosi kuwa hilo lilikiuka makubaliano ya kimataifa na ya ushirikiano wa pande mbili na China itajibu hatua hiyo, bila ya kueleza kwa namna gani.
Hatua hiyo ya kulipiziana kisasi iliongeza mivutano baina ya nchi hizo juu ya masuala ujasusi wa kibiashara na viwanda hadi masuala ya haki za binadamu.
###