Biden alishinda majimbo nane na Sanders manne, likiwemo jimbo muhimu la California, wakati upigaji kura ukitambaa katika ngazi ya kitaifa ambapo kinyang’anyiro kinaendelea katika majimbo kutoka pwani hadi pwani.
Sanders pia ameshinda majimbo ya Magharibi ya Colorado na Utah pamoja na jimbo lake la nyumbani la Vermont upande wa kaskazini mashariki ya Marekani.
Biden, katika kinyang’anyiro cha tatu cha kuwania urais wa Marekani, aliongoza maeneo yote ya Kusini, na hivyo kushinda Virginia, North Carolina, Alabama, Oklahoma, Tennessee na Arkansas, pamoja na Minnesota na Massachusetts.
Mapema Jumatano, Biden na Sanders walikuwa wanachuana kwa karibu huko Texas na Maine, ambapo uchaguzi ni mkali na matokeo bado hayajakamilika. Uchaguzi wa Texas ulishangaza kwa matokeo ya awali ya kitaifa yalionyesha Sanders akiwa anaongoza, lakini ikageuka kuwa ni mapambano jioni Jumanne.
Matokeo hayo yalikuwa kwa ujumla yanafanana na tafiti zilizofanywa kabla ya uchaguzi ikionyesha Biden akishinda majimbo mengi zaidi uchaguzi wa Super Tuesday, lakini Sanders akishinda maeneo yenye wajumbe muhimu kwa siku hiyo, zaidi kutokana na matokeo ya California na Texas.
Sanders ameonyesha kujiamini katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Vermont Jumanne, akisema siyo tu kwamba atakuwa mteule wa chama cha Demokratiki, lakini atamshinda Rais wa Republikan Donald Trump.
“Huwezi kumshinda Trump na siasa zile zile za zamani. Tunachohitaji ni siasa mpya zinazoleta tabaka ya wafanyakazi katika harakati zetu za siasa, zitakazowaleta vijana katika harakati zetu za kisiasa, ambazo mwezi Novemba itawaleta wapiga kura wengi zaidi katika historia ya siasa za Marekani,” amesema Sanders.
Ushindi wa Biden, uliokuja siku tatu baada ya ushindi wa kishindo huko South Carolina, ulielekeza nguvu mpya katika kinyang’anyiro hicho na huenda atachuana na Trump uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba. Biden alishinda uchaguzi wa South Carolina kutokana na kuungwa mkono kwa nguvu zote na wapiga kura Wamarekani weusi.