Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 21:10

HOTUBA YA HALI YA TAIFA: Trump, Pelosi waonyesha uhasama hadharani


Rais wa Marekani Donald Trump akitoa hotuba yake ya tatu ya Hali ya Taifa.
Rais wa Marekani Donald Trump akitoa hotuba yake ya tatu ya Hali ya Taifa.

Rais wa Marekani Donald Trump Jumanne usiku alianza hotuba yake ya tatu ya Hali ya Taifa kwa kuelezea hatua ambazo, alisema, utawala wake umepiga katika kuimarisha uchumi tangu alipoingia mamlakani.

Trump alikuwa akilihutubia taifa kwenye majengo ya bunge ambapo alielezea sera za utawala wake na kusema kwamba alikuwa ametimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni ya kwelekea kwa uchaguzi wa mwaka 2016.

Hata hivyo, punde tu baada ya hotuba hiyo, Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi, akionekana mwenye hasira, alirarua nakala ya hotuba hiyo na kuitupa mezani.

Awali, Trump alishangiliwa na wabunge wa chama cha Republican muda mfupi baada ya kuanza hotuba yake.

"Miaka mingine minne! Miaka mingine minne!" walisema.

Pamoja na kusifia juhudi zake za kuimarisha uchumi, rais huyo, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya kutaka kumwondoa mamlakani, aliguzia masuala mengine kadhaa, ikiwa ni pamoja na sera zake kuhusu elimu, uhamiaji, jeshi la Marekani, ugaidi na nafasi za ajira kwa Wamerkani weusi na wanawake.

Na katika tukio lingine la kushtukiza, Trump alimkaribisha kiongozi wa upinzani wa Venezuela, Juan Guaido, ambaye alikuwa ndani ya ukumbi huo wa bunge.

Aidha Trump aliwatuza baadhi ya wageni walioalikwa, ikiwa ni pamoja na mtangazaji maarufu wa redio Rush Limbaugh, anayefahamika kwa kutetea sera za Warepublican.

Limbaugh alitangaza mapema wiki hii kwamba anaugua saratani ya mapafu.

Mwanzoni mwa hotuba hiyo, tukio lisilo la kawaida lilijiri pale rais huyo alionekana kama alipuuza ishara ya Spika Pelosi, ambaye alikuwa amemnyooshea mkono wa kumkaribisha kwenye jukwaa ili kuanza hotuba yake.

Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi.
Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, Nancy Pelosi.

Trump alipita bila kumwangalia Bi Pelosi na kusimama mbele yake tayari kwa hotuba hiyo.

Hotuba hiyo ilijiri wakati ambapo Wamarekani wamegawanyika kisiasa kwa, hususan kufuatia hatua ya Baraza la Wawakilishi kuwasilisha mashtaka ya kutaka kumwondoa mbele ya baraza la seneti, huku taifa likielekea kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Novemba mwaka huu.

Mchambuzi wa masuala ya siasa Prof Fulbert Namwamba alisema hotuba ya rais huyo ni mkakati tu wa kujitayarisha kwa uchaguzi huo.

"Yote aliyoyasema kwenye hotuba hiyo ni ya kutaka kujipendekeza kwa wapiga kura," alisema Prof Namwamba katika mahojiano ya moja kwa moja kwa njia ya simu na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika.

XS
SM
MD
LG