Sanders ameonyesha kuongoza kitaifa kuweza kuteuliwa kuwa mwakilishi wa chama hicho baada ya ushindi katika majimbo matatu.
Wapinzani wake wanahofia kwamba mgombea huyo aliyejitangaza mdemokrat mwenye mrengo wa kushoto wa kisoshalisti anaweza kushindwa na rais Donald Trump wakati wa uchaguzi wa Novemba 2020.
Katika mjadala huo wa ana kwa ana uliotayarishwa na shirika la televisheni la CBS, Seneta huru wa Vermont Bernie Sanders aliulizwa jinsi atakavyo imarisha uchumi zaidi ya anavyofanya Rais Donald Trump, ikitiliwa maanani kwamba masoko ya hisa ya Marekani yamekuwa yakifanya vyema katika siku za hivi karibuni.
Sanders afafanua sera zake
Seneta Sanders anatoa ufafanuzi : " Mwaka 2019, nyongeza za mishahara ya mfanyakazi wa wastani ilikuwa chini ya asilimia moja. Maisha ya nusu ya watu wetu yanategemea mshahara wa wiki baada ya wiki… Huo sio uchumi unaowasaidia Wamarekani, huo ni uchumi unaowafaidisha asilimia 1 pekee ya wananchi matajiri. Tutaunda uchumi utakao wafaidisha watu wote, sio tu matajiri wanaochangia katika kampeni."
Sanders ameahidi kupanua mpango wa bima ya afya unaowahudumia wazee, utakao pia mhusisha kila mtu bila ya kuzingatia umri.
Lakini wapinzani wake akiwemo Seneta wa Minnesota Amy Klobuchar, wanadai kwamba mpango wake Sanders, utaongeza gharama ya huduma za kijamii kwa ajili ya afya na elimu kwa kiwango kikubwa sana.
Seneta Amy Klobuchar: "Hapana! Hesabu sio sahihi. Kwa hakika Katika kipindi cha televisheni cha 60 Minute, wikendi hii, alisema hataongeza gharama. Niwaambie kwamba mpango wake utagharimu dola trilioni 60. Basi, Je, unafahamu mipango yake yote itagharimu kiasi gani cha pesa?
Lakini kwa upande wake Seneta Sanders amesema :"Hiyo sio kweli."
Naye Seneta Klobuchar amesema : "Hiyo ni mara tatu ya uchumi wa Marekani, sio matumizi ya serikali kuu, uchumi mzima wa Marekani.
Biden amkosoa Sanders
Aliyekuwa Makamu wa Rais Joe Biden, alitumia tukio la mashambulizi ya risasi la mwaka 2015, katika kanisa linalohudhuriwa na idadi kubwa ya watu weusi, Charleston, kukabiliana na Sanders kuhusiana na msimamo wake wa awali kupinga uundaji wa sheria ambayo ingewalazimu watengenezaji wa bunduki kuajibika na mashambulizi ya risasi nchini Marekani.
Biden amesema: "Bernie alipiga kura mara tano kupinga muswada wa Brady na kusubiri kwa mda saa 12. Sisemi kwamba anawajibika kwa vifo vya watu tisa, lakini mshambuliaji hangeweza kupata silaha iwapo mda wa kusubiri kuchunguzwa ungekuwepo, jinsi nilivyokuwa nimependekeza.
Wapinzani wa Sanders pia wamemkosoa kutokana na msimamo wake wa miongo kadhaa kuwahusu viongozi wanaochukuliwa kama madikteta kama Fidel Castro wa Cuba, wakisema utakataliwa na wapiga kura wenye msimamo wa wastan katika baadhi ya sehemu za nchi.
Aliyekuwa meya wa New York Michael Bloomberg, hata alipendekeza kwamba Sanders alikuwa anatumiwa na rais wa Russia Vladimir Putin.
Bloomberg aeleza mkakati wa Rashia
Kwa upande wake Meya wa zamani wa New York Michael Bloomberg alieleza kuwa : "Nadhani kwamba Donald Trump anafikiria kwamba itakuwa vyema zaidi akiwa rais, lakini sidhani hivyo. Vladmir Putin anafikiria kwamba Donald Trump anastahili kuendele akuwa rais wa Marekani na ndio sababu Russia inakusaidia ili ushindwe na Trump”.
Mjadala huo umefanyika siku nne kabla ya jimbo la South Carolina, lenye wajumbe 54 wa Democratic, kuanza kupiga kura ya awali.
Biden ambaye alikuwa mbele katika kinyang’anyiro hicho, ana ushindi mdogo sana mbele ya Sanders katika jimbo la South Carolina, lakini wachambuzi wanasema kwamba Sanders anaweza kushinda jimbo hilo na kumuweka katika nafasi nzuri kuelekea uchaguzi wa jumanne, maarufu kama super Tuesday, ambapo zaidi ya wajumbe 1300 watashiriki.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.