Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 06:00

Afrika Mashariki bado inakabiliwa na maambukizi ya COVID-19


Rais Paul Kagame
Rais Paul Kagame

Katika Kanda ya nchi za Maziwa Makuu na Afrika Mashariki, idadi ya maambukizi nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imefikia 500, baada ya visa vipya 9 kuripotiwa hapo jana mjini Kinshasa.

Hadi Alhamisi ripoti zinaeleza kuwa watu 31 wamefariki DRC, na 65 wamepona.

Maambukizi ya corona yamethibitishwa katika jela ya Ndolo mjini Kinshasa, wafungwa wanne wameambukizwa corona katika jela hiyo tangu Jumanne wiki hii, imesema ripoti ya kitengo cha kupambana na COVID-19 nchini humo.

Katika nchi jirani ya Rwanda, Wizara ya Afya Jumatano imeripoti maambukizi mapya 13, wote hao wakiwa ni madereva wa malori ya kubeba mizigo. Rwanda sasa ina jumla ya wagonjwa 225, walipona ni 98, na hakuna kifo kilichotokea.

Wakati huo huo, Rais wa Rwanda Paul Kagame ameomba nchi za Umoja wa Afrika kuungana katika kuagiza vifaa vinavyohitajika katika kupambana na corona, hasa vifaa vya kupima ugonjwa huo.

Ametoa ombi hilo Jumatano katika mkutano kwa njia ya video na baadhi ya viongozi wa Afrika, mkutano ambao ulikuwa unaongozwa na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, ambae ndie mwenyekiti wa umoja wa Afrika.

Uganda nayo imeripoti visa vipya 2 vya maambukizi. Watu hao mmoja ni raia wa Uganda mwenye umri wa miaka 24, na mwengine ni mkimbizi wa Burundi mwenye umri wa miaka 21. Wawili hao wanaaminika kwamba walikutana na mkimbizi wa Burundi aliegundulika kuwa na corona. Hadi sasa Uganda ina visa 81, wagonjwa 52 walipona, hakuna kifo kilichokwisha ripotiwa.

Nchini Kenya, idadi ya maambukizi imefikia 396. Tanzania pia ilikuwa haijaripoti maambukizi mapya ambapo hadi Jumatano ilikuwa na visa 480. Burundi haijaripoti kisa kipya kwa kipindi cha wiki moja sasa.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Patrick Nduwimana, VOA, Washington.

XS
SM
MD
LG